05 September 2012
Upepelezi kesi ya Dkt. Mkopi wakamilika
Na Rehema Mohamed
UPANDE wa mashtaka umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, upelelezi wa kesi inayomkabili Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dkt. Namala Mkopi, umekamilika.
Wakili wa Serikali Bi. Wila Ahoga, alidai hayo mahakamani hapo jana wakati kesi hiyo ilipoletwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya hakimu Bw. Faisal Kahamba.
Alidai kuwa, kutokana na upelelezi huo kukamilika anaiomba Mahakama hiyo ipange tarehe ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali ambapo Hakimu Kahamba, alipanga Septemba 27 mwaka huu.
Katika kesi hiyo, Dkt. Mkopi anakabiliwa na mashitaka mawili, likiwemo la kutotii amri ya mahakama ya kuzuia mgomo wa madaktari na uhamasishaji mgomo kinyume cha sheria.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, akisaidiana na Ladslaus Komanya, ulidai kati ya Juni 26 na 28 mwaka huu, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa Rais wa MAT, hakutii amri iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Kazi, Juni 26, mwaka huu.
Ilidaiwa kuwa, amri hiyo ilimtaka Dkt. Mkopi kuwatangazia wanachama wake kwamba wamezuiwa kushiriki mgomo kama amri ya awali iliyotolewa na Mahakama hiyo, Juni 22 mwaka huu.
Shitaka la pili, ilidaiwa Juni 27 mwaka huu, jijini Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa mjumbe wa MAT aliwashawishi wajumbe wa chama hicho kufanya mgomo kinyume cha amri iliyotolewa na Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi, Juni 22 mwaka huu.
Mshitakiwa huyo anatetewa na jopo la mawakili wanne, likiongozwa na Isaya Matamba, Dkt. Maulid Kikondo, Dkt. Gaston Kennedy na Dkt. Rugemeleza Nshala.
Dkt. Mkopi yupo nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya dhamana sh. 500,000.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment