05 September 2012
ADC watetea uamuzi wa Hamad kuwa mlezi wao
Stella Aron na Rehema Maigala
CHAMA cha Alliance for Democratic Change (ADC), kimesema si jambo la ajabu kwa Mbunge wa Wawi Zanzibar, Bw. Hamad Rashid Mohamed (CUF), kuwa mlezi wa chama chao wakati yeye ni mwanachama wa chama kingine cha siasa.
Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Said Miraji aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa, Bw. Mohamed hana kadi ya chama hicho.
Alisema kutokana baadhi ya watu kutofahamu malezi, hali hiyo imechangia baadhi ya watoto nchini kuwa na maadili mabaya kwa sababu wazazi wao wameshindwa kuwakemea wanapofanya kosa.
“Sisi ndio tulimuomba awe mlezi wa chama na Mkutano Mkuu ulilidhia hivyo kukubali kwa Bw. Mohamed, si dhambi kama mlezi wetu ndio maana hata watoto wanapaswa kulelewa na watu wote badala ya wazazi peke yao,” alisema.
Alitolea mfano kuwa, kama Bw. Mohamed amefanya kosa vyam vingi vya siasa nchini visingeenda nyumbani kwa mama Maria Nyerere kuomba ushauri kwa sababu ni mwanachama wa CCM.
“Kitendo cha Bw. Mohamed kukubali kuwa mlezi wetu, baadhi ya watu wamekuwa na mtazamo hasi, mbona wakati Bw. Augustine Mrema akiwa NCCR-Mageuzi na Bw. Mabere Marando, walikwenda kuomba ushauri kwa Mwalimu Nyerere, je, nao walifanya makosa,” alihoji Bw. Miraji.
Alisema jambo la msingi kwa vyama vya siasa ni kukaa pamoja, kujenga hoja na kuzisimamia ili ziweze kutengeneza mambo ambayo yatakuwa na faida kwa wananchi badala ya kujenga hoja zisizo na msingi wowote.
Aliongeza kuwa, baadhi ya vyama vya siasa nchini havina uzalendo hivyo kusababisha washindwe kushirikiana na kuombeana mabaya.
Wiki iliyopita chama hicho kilimtangaza Bw. Mohamed kuwa mlezi wao jambo lililozua hisia tofauti kwa baadhi ya watu kikiwemo chama chake cha CUF.
Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi na Mahuasini na Umma wa CUF, Bw. Abdula Kambaya, alisema suala hilo wanaliachia mahakama.
“Sisi tunaiachia mahakama juu ya kesi ambayo Bw. Mohamed ameifungua dhidi ya CUF, baada ya kutangazwa kuwa mlezi wa chama kipya cha ADC,” alisema.
Bw. Mohamed na wenzake 10, walipinga kuvuliwa uanachama wa CUF kwenye Kikao cha Baraza Kuu la chama hicho Taifa ambapo kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment