19 September 2012

Ubalozi wa Marekani Tanzania walaani mauaji ya Balozi Libya


Na Godfrey Ismaely

UBALOZI wa Marekani nchini, umeungana na Rais Jakaya Kikwete kupitia salamu zake alizotoa kwa Rais Barack Obama na viongozi wa dini ya Kiislamu, kulaani mauaji ya Balozi wao nchini Libya, marehemu Christopher Stevens.


Balozi huyo aliuawa kwa kushambuliwa na watu waliovamia ubalozi huo Mashariki mwa Mji wa Benghazi, nchini humo ili kupinga filamu iliyokuwa ikimkejeli Mtume Muhammad.

Akizungumza na Dar es Salaam jana katika hafla fupi ya kukabidhi hundi ya dola za Marekani 106,000 (zaidi ya sh. milioni 155 za Tanzania), Balozi wa Marekani nchini, Bw. Alfonso Lenhardt, alisema nchi hiyo imesikitishwa na mauaji ya balozi wao.

Hundi hiyo ilikabidhiwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uzima kwa Sanaa, Dkt. Vera Pieroth, ili kuendeleza na kuhifadhi vyanzo vya utamaduni katika Nyumba ya Bwanga mjini Pangani.

“Tumeipokea taarifa ya Rais Kikwete na waumini wote wa Kiislamu nchini wakilaani mauaji haya na mashambulizi ya ubalozi wetu nchini Libya suala ambalo linahusishwa na imani za dini.

“Tukiwa (Marekani) kama nyumba ya watu wenye imani zote wakiwemo mamilioni ya Waislamu, Serikali ya Marekani imejitolea kukuza na kuendeleza utamaduni wetu wa amani kwa dini zote,” alisema Balozi Lenhardt.

Aliongeza kuwa, awali Waziri wa Mambo ya Nje nchini humo, Bi. Hillary Clinton, alisema Marekani inalaani vurugu hizo ambazo zilihusishwa na filamu ya upotoshaji ambayo ilisambazwa katika mtandao wa intaneti ili kuchochea maandamano ya kuipinga.

“Filamu hii imekuwa ikichochea maandamano katika mataifa mengine hivyo tutafanya majadiliano kuendeleza utamaduni wetu pamoja na kuendelea kuheshimu imani ya kila mtu,” alisema.

“Ubalozi wetu hapa Dar es Salaam unajivunia kuwa karibu na viongozi wote wa dini, maelewano ya kuridhisha katika masuala ya kitaaluma na kusaidia jamii wakiwemo waumini wa Kiislaumu, hivi ni moja ya vipaumbele vyetu vikubwa,” alisema.

Awali Rais Kikwete alimtumia Rais Barack Obama salamu za rambirambi baada ya kuuawa kwa balozi wao nchini Libya, maofisa wengine, kusisitiza uvumilivu na kufanya majadiliano ya amani.

“Serikali yangu inalaani kuuawa kwa Balozi wa Marekani na maofisa wengine nchini Libya, suala hili linahusishwa na imani za kishirikina, Serikali yetu itafanya kila liwezekanao kuhakikisha haya yaliyotokea hayatokei Tanzania,” alikaririwa Rais Kikwete katika salamu zake kwa Rais Obama hivi karibuni.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uzima kwa Sanaa, Dkt. Pieroth, alisema fedha hizo zitawajengea uwezo mafundi seremala wadogo ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na manufaa zaidi.


No comments:

Post a Comment