19 September 2012

MPR yashauri wananchi kufuatilia matumizi fedha za ruzuku PETS


Na Stella Aron

WAKAZI wa Kata za Kibamba na Mbezi, Dar es Salaam, wameshauriwa kuunganisha nguvu zao ili kufuatilia matumizi ya Fedha za Ruzuku (PETS), zinazotengwa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo hasa ya maji.

Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Kupambana na Kupunguza Umaskini (MPR), Bw. Mngoya Bakari, aliyasema hayo juzi baada ya kumalizika kwa mafunzo ya PETS.

Mafunzo hayo yalihusu maendeleo ya sekta ya maji ambayo yaliandaliwa na Taasisi ya Foundation For Civil Society.

Alisema sababu kubwa ya kuanzishwa MPR ni baada ya kubaini kuwa jamii inakabiliwa na changamoto nyingi hasa suala la maji ambalo limekuwa kero kwa muda mrefu katika kata hizo.

“Tumeona ni vyema kuanzisha taasisi hii ambayo itatumika kama kituo cha kukutana na kujadili namna ya kukabiliana na changamoto za maendeleo hivyo sisi ni daraja ambalo linaiunganisha jamii pamoja na Serikali,” alisema Bw. Bakari.

Mwenyekiti wa MPR, Bw. Godfrey Kafuru, alisema kwa kutambua umuhimu wa maji, wameazimia kutoa mafunzo kwa wakazi wa kata hizo ili waunganishe nguvu na kusimamia fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi hiyo.

“Jamii kubwa inachelewa kupata maendeleo kwa sababu hawajui haki zao msingi, namna ya kuzifuatilia na kuzidai fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi,” alisema.

Bw. Kafuru alisema MPR imelenga kutoa elimu haki za binadamu, misingi ya utawala bora katika nyanja mbalimbalimbali na kufanya utafiti wa kuainisha mahusiano yaliyopo kati ya utawala bora na maendeleo ya kiuchumi.


No comments:

Post a Comment