26 September 2012
Tusipambana na umaskini kwa mazoea
NCHI mbalimbali duniani zinatekeleza mikakati ya kitaifa na kimataifa kupambana na umaskini ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Inaelezwa kuwa, ili mtu apate mafanikio katika tatizo linalomsibu, kwanza lazima ajitambue hivyo kila anayeshiriki kutokomeza umaskini, anapaswa kujua maskini ni nani?
Kuna vipimo viwili vya kumtambua maskini. Wapo wanaosema maskini ni mtu yeyote anayepata kipato chake chini ya dola moja kwa siku. Kipimo kingine hutumiwa na wataalamu wa uchumi ambacho ni kujipatia mahitahi ya lazima.
Mahitaji hayo ni chakula, malazi na mavazi, upande wa chakula, huangaliwa uwezo wa kaya kumudu milo mitatu kwa siku ambapo katika malazi, huangaliwa nyumba wanayoishi familia husika.
Kama haina faragha wala choo, familia hiyo huitwa maskini wa kutupwa. Mavazi nayo hutumika kama kipimo cha kumtambua maskini ambapo familia zinaposhindwa kuwa na nguo safi, nazo huingizwa katika kundi la watu maskini.
Tanzania ni miongoni mwa nchi maskini ambayo hupimwa kutokana na uchache wa pato la Taifa kwa mwaka, matumizi ya kiwango cha chini cha teknolojia, uduni wa huduma za jamii, miundombinu hafifu, madeni, upatikanaji wa maji safi na salama, uwezo mdogo wa kuzalisha katika sekta ya kilimo na viwanda.
Kutokana na vipimo hivyo, Taifa na watu wake ni maskini lakini tunapaswa kujiuliza lakini sisi tunasema kuwa, sababu moja wapo inayochangia Watanzania wengi kuwa maskini ni mtazamo.
Umasikini wa fikra unawafanya Watanzania wengi kuogopa kuingia katika shughuli za maendeleo kwa mfano, mtu ana shamba kubwa lenye miti badala ya kupata utaalamu wa kufuga nyuki ili azalishe asali, anaona bora anunue shoka ili akate mkaa.
Ukataji mkaa ni kazi kubwa ambayo haina tija na kipato chake ni kidogo hivyo upo umuhimu wa kubadili fikra zetu kwani umaskini si maumbile bali jambo la msingi ni kujitambua.
Watanzania wengi wanapambana na umaskini kwa mazoea hivyo kusababisha wengi wao kukosa upeo wa utambuzi jambo ambalo husababisha kutopata tija au ufanisi kidogo katika shughuli za utafutaji riziki.
Kila mwananchi awajibike kufanya biashara inayoendana na kipato chake kwa kujiamini na kulinda mtaji ili aweze uweze kuongezeka na kukuza biashara kama walivyoanza wajasiliamali wakubwa ambao leo hii, wanamiliki kampuni, viwanda na kutoa ajira.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment