26 September 2012
Mtikila shinda kesi ya uchochezi *Awashushua polisi waliotaka kumkamata
Na Rehema Mohamed
MWENYEKITI wa Chama Cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, jana ameshinda kesi ya kuchapisha na kusambaza waraka wa uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete iliyokuwa ikimkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Mchungaji Mtikila ameshinda kesi hiyo katika hukumu iliyosomwa na Hakimu Bw. Ilvin Mugeta, aliyekuwa akiisikiliza.
Hakimu Mugeta alisema, upande wa mashtaka katika kesi hiyo umeshindwa kudhibitisha kesi yao katika vielelezo vyote ambavyo waliviwasilisha mahakamani hapo kama sehemu ya ushahidi.
Upande wa mashtaka katika kesi hiyo ulikuwa na mashahidi wanne ambao ni Bw. Bernette Kipasika, Bw. Daniel Kikunile, Bw. Isack Pingini na Bw. Ebeneza Mrema.
Wakati hukumu hiyo ikitolewa, miongoni mwa hoja zilizozingatiwa ni kuona kama waraka huo ulikuwa ukilenga kuleta chuki, dharau, uchochesi au uasi dhidi ya mamlaka halali ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hoja nyingine ni kama walaka huo unachochochea wananchi kuleta chuki au kuharibu utawala wa haki, muunganiko na hamasa kwa makundi tofauti ya Watanzania.
Katika hoja hizo, Hakimu Mugeta alisema zinaegemea kwenye kifungu namba 31, kifungu kidogo cha tatu cha sheria ya magazeti na kuongeza kuwa, kwa mtazamo wake, waraka wowote wa kusambazwa au maneno ili uwe wa uchochezi, unatakiwa ulete matokeo ya matatizo ambapo mtu kuelezea hisia zake si kuweka uchochezi.
Alisema kifungu cha 18 cha katiba ya nchi, kinaeleza uhuru wa kujieleza ambapo hati yote ya mashtaka, hailelezi ni uchochezi upi uliotokana na kusambazwa kwa waraka huo.
Hakimu Mugeta alisema shahidi wa utetezi Bw. Mpoki Bukuku kutoka Gazeti la Mwananchi alitoa kielelezo cha gazeti hilo la Agosti 6,2009 ambalo lilikuwa na kichwa cha habari kinachosema “Mtikila apiga kampeni kanisani kumpinga JK, achunguzwa na polisi kumwaga sumu Rais asichaguliwe 2010”.
Aliongeza kuwa, shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa habari hiyo ilikuwa ikiripoti kilichotokea jijini Mwanza katika mkutano wa Maaskofu ili kuelimisha jamii na kwamba haikuwa na tatizo lolote kwa sababu polisi hawajalalamika.
Katika kesi hiyo, Mchungaji Mtikila anadaiwa kuwa kati ya Januari 2009 na Aprili 17, 2010, jijini Dar es Salaam, kwa nia ya uchochezi, alisambaza kwa umma waraka uliosomeka “Kikwete kuuangamiza Ukristo', Wakristo waungane kuweka mtu Ikulu”.
Katika utetezi wake, Mchungaji Mtikila alikiri kuandaa waraka huo na kusambaza nakala zaidi ya 100,000 nchini akidai kuwa, waraka huo si wa uchochezi bali unahusu maneno ya Mungu.
Wakati huo huo, Mchungaji Mtikila jana aligoma kukamatwa na polisi waliotaka kumuweka chini ya ulinzi baada ya kutoka mahakamani kusikiliza hukumu yake.
Polisi hao walikuwa na RB namba KMR/RB/1048/12, wakidai Mchungaji Mtikila alitishia kumuua Bw. Gotam Ndunguru.
Akijibishana na polisi hao, Mchungaji Mtikila alisema yeye hawezi kukamatwa na polisi wa vyeo vidogo bali anapohitajika kituoni huwa anapigiwa simu na viongozi wao.
Alidai Bw. Ndunguru anayedai kutishiwa kuuawa ni tapeli na hajawahi kufanya jambo kama hilo.
“Hamuwezi kuondoka na mimi kwa sababu ya vyeo vyenu, hamstahili kunikamata, huwa napigiwa simu na mabosi wenu ninapohitajika polisi na huwa ninaenda mwenyewe, mtanikamataje wakati hamna hati ya kunikamata,” aliwahoji polisi hao.
Baada ya majibizano hayo, Mchungaji Mtikila, alifanikiwa kuondoka eneo la mahakama bila kukamatwa na polisi hao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment