25 September 2012

Tushirikiane kudhibiti utupaji taka hovyo


Na Darlin Said

JIJI la Dar es Salaam ni miongoni majiji makubwa ambalo linaonekana kuwa kitovu cha Biashara  hapa nchini.


Jiji hili linakadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya millioni 4.5 na ongezeko la watu kufikia asilimia 4.3.

Ongezeko la wakazi limesababishwa kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa uhamiaji wa watu kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Kutokana na sababu kumekuwa pia na ongezeko la makazi holela kwa asilimia 70 ya watu wanaishi maeneo yasiyo rasmi.

Mbali na changamoto hiyo jiji limekuwa na kuwa na mandhari isiyoridhisha kutokana na kuzagaa kwa taka na maji machafu kutiririka mitaani na kuonekana kuwa chafu tena lenye harufu mbaya.

Kutokana na hali hiyo viongozi wa jiji  walifanya kongamano la usafi likiwa na lengo la kutafuta njia mbabadala ya kutatua tatizo baada ya kuonekana kufeli kwa mikakati ya kuimarisha usafi tangu zamani.

Katika kongamano hilo moja ya tatizo  waliloliona ambalo linasababisha jiji kuwa chafu ni kutoshirikishwa kwa wananchi katika suala zima na utunzaji wa mazingira pamoja na uboreshaji wa usafi.

Serikali ilishahuriwa kuwapa kipaumbele wananchi katika kusimamia usafi wa jiji kwa kuwapa elimu kwa namna gani wanaweza kushirki katika kuliweka jiji safi.

Mbali na hilo Halmashauri zilishauriwa kuwawezesha wadau wa usafi kwa kuweka utaratibu wa kisheria kuwashirikisha na kuwawezesha kumkamata mtu yeyote anayechafua mazingira kwa njia yeyote ile.

Ili kupunguza kiwango cha taka kinachosafirishwa hadi eneo la dampo taka lazima zitumike kama mbolea kwa wakulima wadogo wadogo.

Hayo yote yatawezekana kama kutakuwepo na ushirikiano nzuri baina ya kampuni, mashirika ya serikali na yasiyo ya serikali kwa kulifanya jiji kupendeza na kuwa mfano wa kuigwa katika nchi yetu.

Kwa mujibu wa takwimu, linakadariwa kuzalisha taka tani 4,25 kwa siku na kati ya hizo kati ya asilimia 26 na 30 ndizo zinazotupwa dampo wakati asilimia 70 huzagaa na kusababisha harufu mbaya.

Pamoja na adha ya uchafu uliokithiri jiji limepoteza mandhari nzuri ukilinganisha na majiji mengine Afrika na Dunia kwa ujumla.

Kutokana na uchafu huo imesababisha watalii kukaa kwa muda mfupi na kukimbilia sehemu nyinine kwa kuhofia afya zao.

Inasikitisha kuona jiji la Dar es Salaam kuwa mfano wa majiji machafu kuliko mengine kwani ni kitovu cha biashara.

Hivyo ni vyema kwa serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kulivalia njuga suala la usafi wa mazingira ili tuondokane na aibu iliyokuwepo.

Mikakati madhubuti lazima iimarishwe na ifuatiliwe ili tatizo hili liishe kabisa kwani Dar es Salaam ndio makao makuu ya biashara nchini.

Pia kila mkazi wa ajitambue kuwa mhusika mkuu wa kutunza mazingira na kuwa mlinzi kwa mwenzake kuhakikisha taka hazitupwi hovyo.

Sera mpya zinatakiwa kuanzishwa ili kurejesha taka na mbolea mboji  ambayo itawapatia kipato wananchi hasa vikundi vya wajasiriamali kuhamasishwa na kuelimishwa kuhusu umuhimu wake.

Hivyo elimu lazima itolewe kabla ya sera hiyo haijatumika ili wananchi waelewe kwa kufanya hivyo itasadisa kwa kiasi kikubwa kutokomeza kuzagaa kwa taka kwani zitaonekana mali kama ilivyo kuwa chupa hivi sasa.

Jiji linapokuwa safi inaijengea heshima nchi na wakazi wake kwani wageni  wengi kutoka nje ya nchi hufikia kabla ya kwenda nchi nyingine.

Mbali na hilo tutaweza kuboresha afya za wakazi hasa watoto wa mitaani na majumbani kwa kuwalinda na magojwa yatokanayo uchafu.

Tukatae uchafu, kila mtu akiwajibika katika hili tutapiga hatua.s
0713 488 448.

No comments:

Post a Comment