25 September 2012

Timu za Magereza zaendeleza ushindi


Na Mwali Ibrahim

MABINGWA watetezi katika mashindano ya Klabu Bingwa ya wavu, timu za Magereza wanawake na wanaume wameendeleza wimbi la ushindi katika michuano hiyo inayoendelea kwenye Ukumbi wa Bwalo, Morogoro.

Wanaume Magereza wameichapa Jeshi Stars kwa seti 3-2 huku wanawake Magereza wakaifunga Jeshi Stars kwa seti 3-0. Mabingwa hao katika mchezo mwingine waliwafunga wenyeji Moro Stars kwa seti 3-0.

Katika michezo mingine iliyochezwa jana kwa wanaume Moro Stars, wameifunga Kilimanjaro kwa seti 3-0, huku Mzinga ikiifunga Kijichi kwa seti 3-2.

Akizungumza kwa simu akiwa Morogoro, Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Chama cha Wavu Tanzania (TAVA), Alfred Selengia alisema mashindano hayo yapo katika hatua ya mtoani na yanatarajia kumalizika kesho.

Alisema timu zote zimepania kunyakua ubingwa wa michuano hiyo, hali iliyosababisha ushindani wa hali ya juu.

"Mashindano ni mazuri na yana upinzani mkali mno, kwani kila timu imejipanga vyema tofauti na myaliyopita, tunaamini tutapata mwakilishi mzuri katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati," alisema.

Bingwa wa mashindano hayo ataiwakilisha nchi katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati, ambayo yatafanyika mwakani.

No comments:

Post a Comment