11 September 2012
Tushiriki kutekeleza miradi tunayowapelekea watu wetu
Na Charles Lucas
MAENDELEO katika jamii yanategemea miundombinu ya uhakika ili kurahisisha uingizaji na uuzaji wa bidhaa muhimu.
Hali inaweza kuwa nzuri kukiwa na uhamasishaji wa viongozi kwa wananchi ili kutambua umuhimu wa kwa na maendeleo.
Kunaweza kuwa na miundombinu mizuri na rasilimali za kutosha lakini usimamizi mbovu hali inayoweza kuzorotesha juhudi za kupiga hatua katika miradi mbalimbali.
Kwa nchi kama Tanzania ambayo kimazingira ina rasilimali nyingi zinazoweza kuwaondoa katika hali ya umaskini na utegemezi unaotokana na kutokuhamasishwa au kutokuwapo kwa sera zenye uhalisia katika utekelezaji ambazo zimekuwa zikiishia katika makongamano na warsha zisizo na ukomo.
Baada ya miongo kadhaa kuanzishwa kwa vijiji vya ujamaa miaka ya 1971 kwa usimamizi wa Rais wa Kwanza Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kama vijiji vya mfano nchini ni Kijiji cha Kwadelo kilichopo Kata ya Kwadelo Jimbo la Kondoa Kaskazini, mkoani Dodoma kimepiga hatua za maendelao.
Miaka kadhaa baada ya uhuru kulikuwapo na kaulimbiu ya uhamasishaji, kama vile, kilimo cha kufa na kupona, kilimo ni Uti wa Mgongo, Siasa ni Kilimo, ambalo lilikuwa azimio la mwisho kule Iringa, ambapo kilianzia shuleni kila shule ilitakiwa kuwa na shamba la mfano na maofisa ugani walitakiwa kuwa shambani si mijini.
Misemo hiyo ilichochea maendeleo ya kilimo kutokana na viongozi wa wakati ule kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa kauli na vitendo, tofauti na sasa kilimo kinashamiri katika makongamano na warsha badala ya shambani.
Katika kuhakikisha kuwa harakati alizozianzisha hayati Baba wa Taifa, alipotembelea eneo hilo mwaka 1968 na kurudi kwa mara ya pili na Mama Maria Nyerere mwaka 1973 ambapo walishirikiana na wananchi katika ujenzi wa miundombinu ya maji madaraja na zahanati ambavyo vyote sasa vipo katika hali mbaya kutokana na kukosa usimamizi.
Kata ya Kwadelo yenye wakazi 10800, shughuli zao ni kilimo na ufugaji kwa baadhi mazao ya biashara ni alizeti, ufuta, na kwa mazao ya chakula ni mahindi na uwele ingawa yapo mazao mengine ambayo yanastawi kwa kiwango kidogo kama mtama, mbaazi na miwa.
Eneo hilo ambalo kwa upande wa kaskazini linapakana na Hifadhi ya Taifa ya Talangire iliyopo Mkoa wa Manyara kutokana ujirani na hifadhi hiyo yamekuwapo mahusiano mazuri kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kata hiyo hali inayosaidia ustawi wa hifadhi na Waziri Kagasheki kupitia wizara amekuwa mstari wa mbele kushiriki kuchangia katika masuala ya maendeleo.
Ili kukabiliana na hali ya kukata tamaa kwa wananchi kulikotokana na viongozi kutotimiza wajibu katika majukumu yao Diwani wa Kata hiyo, Alhaj Omary Kaliati, ameanzisha harakati kuwahamasisha wakazi wa kata hiyo kufufua miundombinu mbalimbali iliyotelekezwa na kusababisha kutofikiwa malengo ya maendeleo.
Diwani huyo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) amejikita katika uhamasishaji wa kilimo huku naye akishiriki katika shughuli hizo kwa kuwa na tofauti na viongozi wengine kwa kulima mashamba ya mfano yanayofikia hekari zaidi ya 300 za mfano tofauti na viongozi wengine ambao hutoa maelekezo kwa wananchi kupitia runinga na machapisho wakiwa ofisini.
Alhaj Kaliati anayetambulika katika kata yake kama 'Kaliati Matrekta' kutokana na kuwawezesha wananchi kujipatia mikopo ya matrekta ili kushiriki mpango wa Kilimo Kwanza kwa vitendo aliounziasha mwaka mwezi Novemba mwaka 2011.
Awamu ya kwanza wakulima walikabidhiwa matrekta Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaj Ally Hassan Mwinyi na hivi karibuni mjane wa Baba wa Taifa Mama Maria Nyerere alikabidhi matrekta 10.
Anasema, mkopaji hulipia nusu ya gharama husika na hurejesha salio katika kipindi cha miaka minne katika kipindi cha mwaka mmoja hulipa mara mbili kipindi cha kilimo na mavuno kipindi cha kilimo fedha hutokana na trekta kulima katika mashamba kwa kukodiwa na wakulima wengine na wakati wa mavuno mkopaji hulipia fedha zilizotokana na shamba lake.
"Ni rahisi kuwaongoza watanzania ikiwa unawasaidia lakini ni vigumu kukusikiliza ikiwa huwasaidii viongozi lazima tuwe mfano miradi tunayowapelea watu wetu tushiriki kuitekeleza," anasema.
Diwani huyo aliyengia madarakani katika uchaguzi wa mwaka 2010 anaongeza kuwa wananchi unaowaongoza ni lazima wakuamini hoyo lisipowezekana nafasi yako ya uongozi haina mashiko kwa sababu utakuwa kiongozi wa ofisi si wananchi.
"Sitalala usingizi huku umaskini ukiwasumbua watu wangu kwani umaskini huchochea chuki hata kwa chama kinachotawala sasa nalazimika kushirikiana katika kila jambo linalohusu maendeleo si katika kata hii tu katika jimbo na mkoa huu wote hatimaye taifa," anasema.
Bw.Kaliati anasema wameweza kupata matrekta zaidi ya 60 kutoka Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) kwa kata hiyo, pia wakulima katika kata zingine za jimbo hili tunaendelea kuwahamasisha na tunatoa mwito waje wajipatie matrekta.
Diwani huyo anasema Kata yake pia ina changamoto nyingi zinazostahili kushughulikiwa ili kuimarisha mshikamano kubwa hasa ni jinsi ya kuwasaidia watu wenye ulemavu kati ya kaya 1478 zilizopo wanawake walemavu ni 18 na wanaume 8 ambao wanahitaji uwezeshaji ili kushiriki juhudi hizo.
Naye kiongozi wa wakulima hao, Bw. Khamis Haji anatoa shukrani kwa serikali kwa kutambua hitaji lao la msingi ingawa anasema msukumo ni mdogo unaosababishwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa ngazi za jimbo na mkoa kuingiza siasa chafu katika utekelezaji ikiwa ni pamoja na kutotoa ushirikiano wa kutosha katika kufikia malengo yao.
Anasema wameweka msukumo katika masuala ya ujenzi wa mabomba ya maji, zahanati na pampu ya maji yenye uwezo wa kusukuma lita 50000 yenye thamani ya sh milioni 16 yeye mwenyewe kwa nafasi yake ametoa marobota 20 ya alizeti na trekta litakalosaidia katika shighuli hiyo.
Kwa upande wa elimu mikakati inafanyika ili kuongeza shule nyingine ya sekondari kutokana na moja iliyopo kuonekana kuzidiwa kutokana na ongezeko la ufaulu katika elimu ya msingi kwa shule nne zilizopo.
"Maadili ya viongozi katika chama anasema chama hakina tatizo kwa sababu sera ni zilezile pengine tatizo ni baadhi ya viongozi kutotimiza wajibu kwa wananchi hii ndiyo inasababisha watu wakione chama kama tatizo na kuongeza kuwa inapaswa kuweka maslahi ya chama badala ya ubinafsi,"
"Tatizo kubwa kwenye eneo hili ni huduma za kijamii kama maji zahanati na barabara ingawa kwa kiasi fulani barabara inapitika baada ya kutengenezwa kwa nguvu za wananchi
tatizo la maji limesababisha watu kadhaa kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu baada ya kushambuliwa na wanyama wakali porini wakati wakisaka huduma hiyo," anasema.
Anasema hata maji yanayopatina katika madimbwi yaliyopo jirani na eneo hilo ambayo si salama yamekuwa yakitumika kwa binadamu na mifugo hali inayohatarisha usalama wa afya zao kutokana hali hiyo baadhi ya familia zimekumbwa na migogoro inayosababishwa na kutumia muda mwingi nje ya nyumba zao hasa kwa wanawake wanapotafuta maji pia anasema tatizo linachangia kupatikana kwa watoto nje ya ndoa.
Pia ameshauri fedha zinazotolewa na serikali kama mfuko wa jimbo zigawanywe kwa uwiano ili zisaidie kuondoa kero hiyo hasa katika eneo ambalo wananchi wamehamasika kuchangia nguvu zao.
Pia tatizo hilo husababisha ugomvi kati ya wafugaji na wananchi ambapo wafugaji huwazuia watu wengine ili kunywesha kwanza mifugo yao katika maeneo ambayo pia wakazi huhitaji maji hayo.
Kutokana na juhudi hizo hivi karibuni diwani huyo aliendesha harambee na kufanikiwa kukusanya zaidi ya sh. milioni 13, huku Wizara ya Maliasili na Utalii ikichangia milioni 10, ambazo zitatumika kununua mabomba mabati na vifaa vingine wananchi pia watatumika kama nguvu kazi ili kufikia mwezi wa Disemba mwaka huu huduma hizo ziweze kuanza kutumika
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment