11 September 2012

Makundi yanadhohofisha vyama vya siasa


Na Suleiman Abeid

NAANZA makala hii kwa kunukuu methali ya kiswahili isemayo,  “Maji yakimwagika hayazoleki,” ni moja ya methali muhimu ikiwa na maana kuwa jambo likiharibika inakuwa vigumu kulitengeneza.


Lengo kubwa la methali hii ni kutahadharisha jamii kuchukua tahadhari mapema kabla ya jambo lolote halijaharibika na ndiyo walitumia mfano huo wa maji yanapomwagika huwa siyo rahisi kuyazoa chini.

Kwa kipindi kirefu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kumekuwepo na suala la wanachama wake kugawanyika kimakundi hali ambayo imekuwa ikikiathiri chama hicho na kuchangia kwa kiasi kikubwa kunufaisha vyama vya upinzani.

Kuibuka kwa makundi ndani ya chama tawala kulishika kasi  baada ya kukamilika kwa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM kwa ajili ya kuwapata wagombea watakaokiwakilisha chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Katika kipindi hicho kuliibuka kambi mbalimbali zikiwa na lengo moja la kuhakikisha safu ya wagombea wake ndiyo wanaoshinda katika kila nafasi walizokuwa wamegombea ambapo pia mchezo mchafu wa kupakana matope kwa tuhuma za ovyo ndipo ulipoibuka.

Pamoja na wito wa mara kwa mara wa viongozi wa CCM kuwataka wana CCM kujiepusha na suala la makundi lakini wito huo umeonekana kama vile ni kumpigia gita mbuzi na kumlazimisha acheze hali inayochangia kuendelea kwa mnyukano wa wana CCM wenyewe kwa wenyewe.

Matukio ya hivi karibu wilayani Nzega mkoani Tabora kati ya Bw. Khamis Kigwangala na Bw. Hussein Bashe kutoleana silaha mbele ya kadamnasi wakiwa wote ni wafuasi wa chama kimoja yanaashiria hali ya sintofahamu ndani ya CCM iwapo hatua za haraka za kurekebisha hali hiyo hazitochukuliwa.

Katika tukio hilo hali ya makundi ndani ya CCM ilijionesha wazi baada ya pande mbili zilizokuwa zikiwaunga mkono kuonesha chuki za wazi kati yao huku kila upande ukidai upande wa pili ndiyo uliokuwa na kosa na unastahili kuadhibiwa.

Ni wazi kwamba uhasama uliosababishwa na tukio hilo hautoishia hapo ikizingatiwa limetokea mwanzo tu wa mchakato wa kuelekea katika uchaguzi wenyewe. Swali hapa ni kwamba, kama hali ndiyo hiyo kwenye hatua za awali za uchukuaji wa fomu, je, itakuwaje baada ya uchaguzi kumalizika?

Hapa mtu anatakiwa kupeleka mawazo yake mbele kuona kitu gani kinachoweza kutokea baada ya kukamilika kwa uchaguzi huo wa CCM huku upande mmoja mgombea wake akiwa ameangushwa? ni wazi kundi la walioshindwa halitoridhika, je,  hali itakuwaje?

Nzega ni wilaya moja tu ambayo habari zake katika mchakato wa uchukuaji fomu za kuwania nafasi mbalimbali ndani ya CCM zimeweza kusikika, lakini hali katika wilaya nyingi haitofautiani na wilaya hiyo, maana hivi sasa kila mgombea anajipanga kuandaa kundi la kumsaidia katika kampeni ili aweze kushinda nafasi anayogombea.

Wakati mchakato wa uchaguzi katika ngazi ya mashina, matawi na kata ukiwa umekamilika tayari kuna malalamiko kila kona ya baadhi ya wagombea walioshindwa wakilalamikia mchezo wa faulo uliofanyika na kusababisha waangushwe katika chaguzi hizo.

Lakini utafiti umeonesha kuwa baadhi ya makundi yaliyokuwepo katika mchakato wa kura za maoni kwa ajili ya kuwapata wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge yamefufuka upya kwa kila kundi kukamia kuliangusha lingine, hali ambayo tayari imeleta mushkeli mkubwa katika maeneo mengi.

Pamoja na wito uliokuwa ukitolewa mara kwa mara na viongozi wakuu wa kitaifa kuwataka wanachama kuvunja kambi walizokuwa nazo katika kipindi cha chaguzi zilizopita lakini hali imeonekana kuwa tofauti baada ya kambi hizo kuanza kujipanga upya huku nyingine zikituhumiwa kupanga safu yake ya viongozi.

Wilaya ya Shinyanga mjini matokeo ya uchaguzi wa viongozi wa ngazi ya kata katika baadhi ya kata wilayani humo yamepingwa na baadhi ya wagombea walioshindwa ambapo katika moja ya kata hizo inadaiwa baadhi ya viongozi walipanga safu ya viongozi wanaotakiwa kuchaguliwa.

Baadhi ya wanachama katika kata hiyo waliozungumza na mwandishi wa makala hii walidai kwamba mmoja wa viongozi ngazi ya kata ambaye pia alikuwa miongoni mwa wagombea alidiriki kusambaza karatasi zenye namba ya majina ya wagombea kwa kuwaelekeza wapiga kura ni wagombea gani wanaotakiwa kuchaguliwa.

Wana CCM hao wanadai kwamba sehemu kubwa ya wagombea waliotakiwa kuchaguliwa ni wa kambi moja ambayo tangu ngazi ya matawi ilikuwa ikipinganiwa kuhakikisha wagombea wake wanashinda huku wale wa kambi nyingine wakijikuta wakiangushwa katika nafasi zote walizogombea.

“Kwa kweli tatizo la makundi ndani ya chama chetu lisipopatiwa tiba ya haraka litaendelea kutuathiri kwa kiasi kikubwa, leo hii mtu anadiriki kukiuka waziwazi taratibu za uchaguzi kwa lengo tu la kuhakikisha kambi yake inachaguliwa na hivyo kuweza kupanga safu ya viongozi wanaowataka,”

“Tulimuonesha msimamizi wa uchaguzi katika kata yetu mchezo huo mchafu, lakini katika hali ya kushangaza hata yeye hakuweza kutusaidia, na kweli baada ya matokeo kutangazwa wagombea wote waliotakiwa kuchaguliwa ndiyo walioibuka na ushindi, hali hii imetusikitisha sana,” anaeleza mwanachama huyo. (Jina tunalo).
Ni wazi kwamba vikao vya ngazi ya juu vinapaswa kutumia busara katika kuyapatia ufumbuzi majibu ya wagombea wanaoshindwa katika chaguzi kwa kuchambua ukweli wa malalamiko yao na kama kuna ukweli basi si vibaya chaguzi zikafanyika upya ili kuondoa utata.

Iwapo viongozi wa chama na vikao ngazi za juu havitaona umuhimu wa kushughulikia malalamiko ya kupinga matokeo ya uchaguzi katika ngazi mbalimbali kuanzia matawi hadi mkoa ipo hatari kundi la watu wanaolalamika kugeuka kuwa mamluki hatari ndani ya chama.

Tafiti zinaonesha kwamba maeneo mengi nchini Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho chenye wafuasi wengi, lakini inashangaza ni vipi vyama vya upinzani vimekuwa vikapata ushindi mkubwa huku chama tawala kikianguka.  Ni dhahiri kuwa ushindi huo huchangiwa kwa kiasi kikubwa na wanachama wenyewe.

Mbunge wa zamani wa jimbo la Busega, Dkt. Raphael Chegeni, hivi karibuni akirejesha fomu za kuwania nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) amesema makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yamekidhoofisha kwa kiasi kikubwa chama chake.

Dkt. Chegeni alitahadharisha kwamba iwapo suala la makundi ndani ya CCM halitopatiwa ufumbuzi wa haraka linaweza kuchangia kukiangusha katika uchaguzi mkuu ujao na kushauri wana CCM kufanya mabadiliko ya kweli ndani ya chama chao kupitia uchaguzi  mwaka huu.

Kwa upande wake mmoja wa watendaji wa CCM wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Bw. Marco Charles anasema suala la makundi katika kipindi cha uchaguzi ni jambo lisilokwepeka ambalo hata hivyo lipaswa kutumika vizuri.

Anasema,  “Makundi katika kipindi cha uchaguzi hayakwepeki, lakini wana CCM wanapaswa kuwa makini kuhakikisha baada ya kumalizika kwa uchaguzi wanarejea na kuwa kitu kimoja na kukitetea chama hicho katika uchaguzi mkuu unaohusisha vyama vingi nchini.”

Moja ya njia ambayo inaweza kusaidia kupunguza tatizo la makundi katika kipindi cha uchaguzi ni kusikiliza malalamiko yote yanayowasilishwa mara baada ya uchaguzi na kuyatolea uamuzi wa haraka ili kuuridhisha upande unaolalamika na ni muhimu uamuzi unaotolewa uwe ni wa kweli na wa haki.

Kwa kufanya hivi ni wazi kwamba moja ya madhumuni ya CCM yaliyotajwa ndani ya katiba ya chama hicho Ibara ya tano kifungu cha kwanza kisemacho, “Kwa hiyo malengo na madhumuni ya CCM yatakuwa yafuatayo; kushinda katika uchaguzi wa serikali kuu na serikali za mitaa Tanzania Bara," yatakuwa yametimia kikamilifu.

Pia ni muhimu wanachama wakaizingatia katiba yao katika kila eneo ambalo watakuwa wakitekeleza majukumu ya kichama kwa kuhakikisha wanasema kweli daima na uongo na fitina vinakuwa mwiko kwao, rejea Ibara ya nane ya katiba kifungu cha kwanza hadi cha tano.

Viongozi wa CCM wana wajibu kuhakikisha wanatumia nguvu, juhudi na maarifa yao kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la makundi kwa vitendo badala ya kuishia kutoa matamshi ambayo nyuma yake hakuna utekelezaji wowote unaofanyika.

Akizungumzia suala la makundi miongoni mwa wana CCM, Naibu waziri wa Nishati na Madini nchini, Bw. Stephen Masele anasema pamoja na kwamba makundi hayaepukiki katika kipindi cha kampeni lakini ni muhimu yasichangie mgawanyiko ndani ya chama.

“Makundi kama makundi katika kipindi cha chaguzi mbalimbali hayakwepeki, lakini ni muhimu  tukahakikisha kwamba yanatumika katika kipindi hicho tu, baada ya hapo watu wanarejea kuwa kitu kimoja kwa kuachana nayo,”

“Mmoja wetu anaposhinda upande wa pili ukubali matokeo, na tushikamane na mshindi katika kukijenga chama, na hata tunapoingia katika chaguzi za kiserikali, wote tuwe kitu kimoja badala ya kugeuka kuwa mamluki, ni hatari kwa uhai wa chama chetu,” anaeleza Bw. Masele ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini.






No comments:

Post a Comment