11 September 2012

Tunaunga mkono kauli ya Sumaye kupinga rushwa


JANA Waziri Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, aliitaka Serikali iwajibike kudhibiti mianya ya rushwa ambayo inawanufaisha watu wachache kwa masilahi binafsi.

Bw. Sumaye aliyasema hayo Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 20 ya Chuo Kikuu Huria nchini (OUT) na kusisitiza kuwa, rushwa ni adui wa haki na maendeleo hivyo Serikali inapaswa kuweka mkakati wa kuitokomeza.

Alisema Taifa lolote duniani lisipodhibiti rushwa haliwezi kupiga hatua ya maendeleo kutokana na watu wachache kutumia rasilimali za nchi kujinufaisha.

Sisi tunaunga mkono uali yake kutokana na ukweli kwamba, tatizo la rushwa ni kirusi hatari ambayo kinatembea katika sekta mbalimbali nchini.

Upo umuhimu mkubwa wa Serikali kukomesha rushwa kutokana na madhara yake kwa Taifa kama Tanzania ambalo wananchi wake wanakosa fursa ya kutumia rasilimali zilizopo kujikomboa kimaisha.

Madhara hayo yanapaswa kuisukuma Serikali kuweka mikaakati mbalimbali ya kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa kwani rushwa inaathiri maendeleo ya mtu binafsi, familia na Taifa.


Vitendo hivyo vinajumuisha matumizi mabaya ya madaraka kwa manufaa binafsi, inawafanya viongozi wa umma na sekta binafsi hutumia madaraka waliyonayo kinyume cha sheria ili kujinufaisha.

Watu wanaojihusisha na vitendo hivyo, wanawanyima wananchi mategemeo ya kuwa na maisha bora, kuwakosesha elimu, huduma bora za afya, chakula, maji na mahitaji mengine ya msingi.

Rushwa inachochea makosa ya jinai yanayovuka mipaka, kuvunja amani, utulivu na inaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wakati mwingine husababisha kupungua ubora wa bidhaa zinazozalishwa viwandani.

Imani yetu ni kwamba, rushwa husababisha mapato ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kupungua hivyo kupuguza uwezo wa Serikali kutoa huduma kwa wananchi na kutekeleza malengo ya kuboresha miundombinu ya nchi.

No comments:

Post a Comment