18 September 2012

TFF yafuta kamati ya uchaguzi TAREFA


Na Mwali Ibrahim

KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), imeifuta Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Soka Mkoa wa Tabora (TAREFA), kutokana na kutokukidhi vigezo vya uchaguzi na kusababisha kuvurugika kwa uchaguzi wa chama hicho.


Kamati hiyo imetoa maamuzi yao kupitia kikao kilichokaa Septemba 15 , mwaka huu na kubaini mapungufu hayo na kuwataka viongozi wa chama hicho kuteua kamati mpya ya uchaguzi kabla ya Septemba 24.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Ofisa Habari wa TFF, Bonifance Wambura imemnukuu Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Hamidu Mbwezeleni kuwa, Kamati hiyo imejiridhisha kuwa Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA haina uwezo wa kusimamia majukumu ya uchaguzi wa TAREFA na kutozingatia kikamilifu matakwa ya Kanuni za Uchaguzi ya Wanachama wa TFF.

Alisema,maamuzi hayo wameyachukua kwa kufuata katiba ya TFF Ibara ya 49(1) na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF Ibara ya 10(6), 26(2) na (3) na imefuta mchakato wa uchaguzi wa TAREFA na mchakato huo utaanza upya Septemba 25 na  uchaguzi utafanyika Novemba 4, mwaka huu.

Kamati hiyo pia ilibaini kuwa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Njombe (NJOREFA) uongozi wake wa  muda haukutoa ushirikiano wa kutosha kuiwezesha Kamati yake ya uchaguzi kuanza mchakato wa uchaguzi kwa tarehe iliyokuwa imepangwa na hivyo kusababisha kuchelewa kuanza kwa mchakato huo wa uchaguzi wa mkoa huo mpya.

Kamati imebaini kuwa pia kutokana na changamoto za kiuongozi zinazoukabili mkoa huo mpya, mchakato wa uchaguzi ulioanza Septemba 2, haukuzingatia kikamilifu Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.

Kutokana na kasoro hizo za msingi, mchakato wa uchaguzi wa NJOREFA utaanza upya Septemba 18, 2012 ukizingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.

Uchaguzi wa NJOREFA utafanyika Oktoba 28, mwaka huuLakini kamati hiyo imedai kuwa Vyama vya Mpira wa Miguu mikoa ya Manyara (MARFA) na Kilimanjaro (KRFA) Uchaguzi wa MARFA na KRFA utafanyika Septemba 22 kama ulivyopangwa.

"Kamati inavishauri vyama wanachama wa TFF kuzingatia ratiba ya uchaguzi na Kanuni za uchaguzi za Wanachama wa TFF wakati wote wa michakato ya uchaguzi wa viongozi wa vyama vyao. Viongozi walioko madarakani wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa Kamati za Uchaguzi kama ilivyoianishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi," alisema.

No comments:

Post a Comment