18 September 2012

Malinzi kubariki mashindano ya ngumi taifa leo


Na Mwali Ibrahim

MWENYEKITI Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Deoniz Malinzi leo anatarajia kubariki mashindano ya Taifa ya Ngumi za Ridhaa yaliyoanza kutimua vumbi jana jioni katika Uwanja wa ndani wa Taifa, Dar es Salaam.


Hadi sasa ni mikoa 18 ambayo imejitokeza kushiriki katika mashindano hayo ,ikiwa ni pamoja na kupima uzito zoezi lililofanyika jana sambamba  na upangaji wa ratiba wa mashindano hayo ambayo yanategemewa kubeba sura ya taifa.

Katika mashindano hayo mikoa mbalimbali  imejitokeza kuthibitisha kushiriki mashindano hayo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga alisema mwaka huu mikoa imeitikia wito kwa kiasi kikubwa, ambapo ni mikoa mingi ilithibitisha kushiriki awali lakini hadi jana mikoa mingine ambayo ilikuwa bado haijathibitisha iliwasili na tayari mabondia wake walipima uzito.

 "Yaani hapa kuna mikoa ilikuwa haijathibitisha lakini imeweza kuthibitisha dakika za mwisho, na kuwahi kupima uzito lakini pia ipo mikoa ambayo imethibitisha na imechelewa kupima uzito lakini katika mashindano ya ngumi hilo limekuwa ni jambo la kawaida na tunategemea mikoa hiyo itakuja na kushiriki," alisema.

Mashindano hayo yanalenga kusaka timu mpya ya taifa ambayo itakuwa ikichuana katika mashindano mbalimbali, na pia itakuwa na sura ya  wachezaji kutoka katika mikoa mbalimbali katika kila uzito.

No comments:

Post a Comment