24 September 2012

Tendwa: CHADEMA susieni na ruzuku *Lipumba adai CCM inakandamiza upinzani


Na Goodluck Hongo

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Bw. John Tendwa, amehoji msimamo wa Chama cha Demokrasia na Mendeleo (CHADEMA), kukacha mkutano ambao umeshirikisha viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa nchini.

Alisema kama CHADEMA ina msimamo wa kweli, wawe tayari kususia na ruzuku inayotolewa na ofisi yake.

Bw. Tendwa aliyasema hayo Dar es Salaam jana na kuongeza kuwa, vyama vyote vya siasa vilivyopewa mwaliko wa kushiriki mkutano huo vimeitikia wito wake isipokuwa CHADEMA, ambacho kilishaahidi kususia shughuli zote ambazo ataziandaa.

Alisema si vizuri kususia mkutano ambao ameuandaa ili kuangalia wajibu wa vyama vya siasa nchini na Jeshi la Polisi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

“Mimi ndiye ninayetoa ruzuku kwa vyama vya siasa vyenye wabunge sasa wapo tayari kuisusia?..hii ni mara ya pili tangu tumeanzisha utaratibu wa kukutana na kujadiliana.

“Mkutano huu utatupa sura ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 jinsi utakavyokuwa na lengo kuu ni kudumisha amani, usalama wa nchi, wajibu wa Jeshi la Polisi na vyama vya siasa kukuza demokrasia ya vyama vingi,” alisema Bw. Tendwa.

Aliongeza kuwa, mkutano huo pia umeshirikisha wadau wengine likiwemo Jeshi la Polisi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Wahadhiri kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam na wawakilishi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.

Mada nne zilijadiliwa katika mkutano huo ambapo baadhi ya watoa mada walitoka Jeshi la Polisi nchini na Taasisi ya Shule ya Uandishi wa Habari Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (IJMC),

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema chama kilichoshika dola kinakandamiza upinzani ili waendelee kubaki madarakani.

“Hawataki kuona upinzani unashika madaraka na vyombo vya dola vinapaswa kuacha kukandamiza uhuru wa vyama vya siasa ili walioshika dola waendelee kubaki madarakani.

“Wananchi wanatishiwa bunduki na mfano mzuri ni uchaguzi mdogo wa Uwakilishi Jimbo la Bububu, Zanzibar ambapo polisi walikuja na bunduki wakiwa wamevaa kininja na kuziba sura zao, siamini kama CCM itakubali kutoka madarakani,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Bi. Angellah Kairuki, alisema vyama vya siasa na Jeshi la polisi vina wajibu wa kufanya kazi kwa kuelewana, kuvumiliana na kuheshimiana.

Alisema lengo ni kutekeleza majukumu yao kwa wananchi ili kulinda amani iliyopo na kuwataka viongozi wa vyama vya siasa kutimiza wajibu wao na kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuleta maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Akitoa mada katika mkutano huo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, alisema ni kazi ya wanasiasa kutoa elimu kwa wanachi ili kulinda amani iliyopo badala ya jukumu hilo kuachiwa jeshi hilo pekee.

“Baadhi ya tafiti zilizofanywa zimebaini kuwa, kati ya watu 10 mmoja ndie anayejua kazi ya kulinda amani ni jukumu la jamii nzima na tisa wanaamini jukumu hilo ni la Jeshi la Polisi.

“Wakati mwingine polisi tunabanwa hadi kushindwa kutoa maelezo, mimi ni Muislamu lakini wapo wataosema nimewaachia Waislamu wenzangu, kabila langu ni Mchaga, ukiwaachia watu wa kamabila mengine utasikia kawaachia ndugu zake wa kabila moja,” alisema.

Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Bw. Robert Manumba, alisema kuanzia Julai 2011, jeshi hilo lilipokea maombi ya kufanya mikutano na maandamano 1,668 na kati ya hiyo, 110 ilizuiliwa kwa sababu mbalimbali.

Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bw. Bansen Bana, alisema Hayati Mwalimu Juluas Nyerere alisema; “Utii bila uhuru ni utumwa na uhuru bila utii ni uwendawazimu”.


No comments:

Post a Comment