24 September 2012

Serikali imenitelekeza-Mhagama



Na Joseph Mwambije, Songea

SERIKALI inadaiwa kumtelekeza mpiania Uhuru wa Tanganyika aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali, Chama cha TANU na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Joseph Mhagama.

Bw. Mhagama (75), maarufu kwa jina la 'Lilikuliku', amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kupata msaada wowote kutoka serikalini wala kutembelewa na viongozi wa chama na Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo kwa niaba ya mumewe, Bi. Eva Komba ambaye ni mke wa Bw. Mhagama, alisema mume wake anasumbuliwa na maradhi mbalimbali.

“Mume wangu ana tatizo la kibofu cha mkojo, kwikwi na uti wa mgongo hivyo hulazimika kulala muda mrefu,” alisema Bi. Komba ambaye anadai kusoma darasa moja na Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda katika Shule ya Kati Peramiho.

Alisema mumewe alizaliwa mwaka 1937, Kijiji cha Njoomlole, Wilaya ya Namtumbo, mkoani hapa na baada ya kumaliza shule, aliajiriwa kama Bwana Shamba wa Wilaya ya Songea.

Mwaka 1963 hadi 1970, alikuwa Katibu wa TANU,Wilaya ya Songea, mwaka 1965 aligombea ubunge wa Jimbo la Songea Kaskazini akichuana na marehemu Oscar Kambona.



Alisema mwaka 1981, mumewe alichaguliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, mwaka 1983 akarudi Songea kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo na kustaafu mwishoni mwa mwaka huo.

No comments:

Post a Comment