05 September 2012
Tanzania Mwenyekiti mkutano Baraza la Mawaziri-AMCEN
Na Rehema Maigala
TANZANIA itakuwa Mwenyekiti wa mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wa Mazingira wa Nchi za Afrika (AMCEN) utakaofanyika Septemba 10 hadi 14 jijini Arusha mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa Habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dkt. Terezya Huvisa alisema mkutano huo unatarajiwa kuwa na wajumbe 350 ambapo idadi hiyo inajumuisha washiriki kutoka nchi zote za bara la Afrika na baadhi kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
Dkt. Huvisa alisema madhumuni ya mkutano huo ni kutathmini utekelezaji wa makubaliano ya mkutano wa 13 uliofanyika Bamako, Mali na jinsi bara la Afrika lilivyojiandaa kutekeleza maamuzi ya mkutano wa maendeleo endelevu uliofanyika Rio de Janeiro huko Brazir.
Alisema kuwa AMCEN ilianzishwa kwa ajili ya kusimamia masuala ya hifadhi ya mazingira katika Bara la Afrika na kuhakikisha mahitaji ya msingi ya binadamu yanapatikana kwa njia endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho na kutoa miongozo mbalimbali ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa maazimio ya kamisheni ya maendeleo endelevu na mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa inayohusu hifadhi ya mazingira.
Hata hivyo Dkt. Huvisa alisema kuwa AMCEN imewapatia faida ya ushiriki katika kuandaa na kutekeleza programu na miradi mbalimbali, kuanzisha mpango kazi wa mazingira kwa ajili ya maendeleo ya Afrika, kuwa na msimamo wa pamoja katika ngazi ya kimataifa katika masuala ya usimamizi wa mazingira yenye masilahi kwa Afrika.
Dkt. Havisa alisema kuna mradi tayari umeanzishwa ambao umeanza Mei mwaka huu mpaka 2016 wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi katika Pwani za Pangani, Bagamoyo, Rufiji na Zanzibar wenye thamani ya dola za Marekani milioni 3.3, lengo ni kujenga ukuta katika Bahari ya Hindi maeneo ya Pangani na kuchimba visima vya maji baridi kwa matumizi ya binadamu maeneo ya Bagamoyo.
"Faida ya Tanzania kuwa Mwenyekiti wa AMCEN kwa miaka miwili,itasaidia kuongeza fursa za upatikanaji wa fedha zitakazoshughulikia changamoto za masuala ya hifadhi ya mazingira," alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment