05 September 2012
Polisi watakiwa kuacha kutumia nguvu
Neema Kalaliche na
Lulu Malenda
JESHI la Polisi nchini limeshauriwa kubuni mbinu za kisasa katika kukabiliana na vurugu zinazotokana na harakati za kisiasa na kuacha kutumia nguvu ambazo zinasababisha madhara.
Kauli hiyo imetolewa katika taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, Bw.Hezron Kaaya, ambapo alisema matumizi ya silaha kamwe hayawezi kuwa suluhisho la vurugu badala yake wanajenga usugu wa wananchi.
Bw.Kaaya alisema, matukio ya vurugu ambayo yanaonekana leo ndiyo ambayo baadaye yanakuja kuzaa machafuko katika nchi na haya yameshuhudiwa yakitokea katika nchi nyingi na TUCTA hatutapenda nchi yetu ifikie huko.
Pia TUCTA imelaani vikali mauaji ya mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Bw.Daudi Mwangosi baada ya kutokea vurugu kati ya polisi na wafuasi wa CHADEMA mkoani Iringa.
"Kama mauaji haya yamefanywa na Jeshi la Polisi basi linaipeleka nchi pabaya kwa kuwa wananchi hawawezi kuendelea kuvumilia kuachwa wajane na yatima kutokana na ndugu zao kuuawa na polisi kwa sababu zisizoeleweka," alisema Bw.Kaaya.
Aidha katika taarifa hiyo Bw.Kaaya alionesha masikitiko yake na kusema marehemu alikuwa mfanyakazi ambaye alikuwa akitekeleza wajibu wake wa kutafuta habari kwa mujibu wa kazi yake, kinachosikitisha ni kwamba ni vurugu gani aliyofanya mpaka akatishwe maisha yake kinyama.
Alisema kuwa upande wowote ambao utajulikana umehusika katika mauaji hayo ya mwandishi uwajibishwe na ubebeshwe jukumu la kuilipa fidia familia ya marehemu.Wanasiasa wawe makini na kuhakikisha wanashirikiana na walinzi wa usalama kwenye harakati zao za kisiasa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment