05 September 2012

Shahidi wa tano biashara haramu atoa ushahidi


Na Rehema Mohamed

SHAHIDI wa tano katika kesi ya biashara haramu ya kusafirisha binadamu ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mshtakiwa wa kesi hiyo, Bw.Salim Ally alikamatwa Februari 3, mwaka huu baada ya kukiuka masharti ya dhamana.

Shahidi huyo Kamishna Msaidizi wa Polisi, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi ASP Afwilile Mponi alieleza hayo jana mahakamani hapo wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu, Bw.Ilvin Mugeta huku akiongozwa na wakili wa serikali Bw.Prosper Mwangamila.

Mshtakiwa wa kesi hiyo ambaye ni Mfanyabiashara wa Mjini Arusha, anadaiwa kuwasafirisha Bw. Abduswamad Zakaria, Bw. Hamidu Biabato, Bw. Raufu Biabato na Bw.Sadick Almas kutoka nchini kwenda Yemen na kuwafanyisha kazi za kitumwa.

Shahidi huyo alidai kuwa awali mshtakiwa huyo alikamatwa Oktoba 3, mwaka jana baada ya mlalamikaji Bw.Abdulswamad Zakaria kuja kutoa taarifa polisi na kuchukuliwa maelezo na kisha kuachiwa kwa dhamana.

Alidai kuwa baada ya kupewa dhamana hiyo mshtakiwa huyo alitakiwa kuripoti tena Makao Makuu ya Polisi Novemba 3, mwaka jana, lakini alikaidi na ndipo alipoandika barua ya kulitaka Jeshi la Polisi Mjini Arusha kumkamata mshtakiwa huyo.

Katika hatua nyingine shahidi huyo alidai kuwa Septemba 23 akiwa ofisini kwake alikuja kijana alijemtaja kwa jina la Bw.Abdulswamadu Zakaria na kumlalamikia kuwa Agosti 2010 yeye na wenzake watatu walisafirishwa na Bw.Salim Ally kwenda Yemen kufanya kazi ya mkataba.

Alidai kuwa, kwamujibu wa Bw.Zakaria walipofika Yemen, Bw.Ally alikiuka makubaliano hayo na badala yake kuwafanyisha kazi bila malipo pamoja na kuwanyang'anya hati zao za kusafiria.

Aliongeza kuwa baada ya kupata taarifa hiyo aliunda timu ya upelelezi ambao waliwahoji walalamikaji wote pamoja na mshtakiwa wa kesi hiyo.Kesi hiyo itaendelea leo.



No comments:

Post a Comment