05 September 2012

'Taifa litaingia katika janga la ukame'



Na Ramadhan Libenanga, Morogoro

UKOSEFU wa nishati mbadala ya kuwafanya wananchi waache kukata miti ili kuchoma mkaa, kutalifanya Taifa liingie katika janga kubwa la ukame kutokana na uharibifu wa mazingira.

Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Dkt. Felician Kilahama, aliyasema hayo mjini Morogoro mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na waandishi wa habari ili kuelezea uharibifu wa mazingira ambao unafanywa na wafanyabiashara katika maeneo mengi nchini.

Alisema kasi ya ukataji miti ovyo na uchomaji misitu, inaongezeka kwa zaidi ya asilimia 48 hali inayoweza kulifanya Taifa likumbwe na ukame katika maeneo mengi.

Aliongeza kuwa, hali hiyo inatokana na ukosefu wa nishati mbadala ya kupikia hivyo wafanyabiashara hulazimika kuingia katika misitu ya asili na kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa.

“Nasikitika sana hasa ninapoona maeneo ya barabarani kuanzia Chalinze hadi Segera, Ruvu kuja Morogoro, Dodoma kwenda Morogoro, biashara ya mkaa inafanyika kwa uwazi mkubwa.

“Wafanyabiashara hawana vibali hali inayohamasisha ukataji miti ovyo, Maofisa Misitu msikae zungukeni maeneo haya ili kuangalia uharibifu wa mazingira,” alisema.

Alisema sheria za usimamizi wa sera ya mazingiza ziko wazi bali tatizo lipo katika utekelezwaji na kuiomba Serikali na taasisi mbalimbali, kuona suala la uharibifu wa mazingira kuwa ni janga la kitaifa kwani linaweza kuleta madhara makubwa kama litaendelea kufumbiwa macho wakati misitu ikiteketea.

No comments:

Post a Comment