05 September 2012
Simba, Yanga kuonekana Dunia nzima
Na Zahoro Mlanzi
WACHEZAJI wa miamba ya soka nchini, timu za Simba na Yanga, watapata fursa ya kuonesha vipaji vyao barani Afrika na duniani kwa ujumla kupitia Supersports.
Hatua hiyo imekuja baada ya Kampuni ya Multichoice kupitia kituo chake cha Supersports kutaka kuonesha 'live' mechi ya Ligi Kuu ya watani hao wa jadi itakayopigwa Oktoba 3, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mbali na mechi hiyo, kituo hicho kitaonesha pia mechi nyingine nne 'live' kwenye mpango wao wa majaribio katika kuhakikisha msimu wa 2013/2014 wanakuwa ni moja ya kampuni inayodhamini Ligi Kuu Bara.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema shirikisho hilo limeingia makubaliano ya awali na kituo hicho kwa kuanza kuonesha baadhi ya mechi katika ligi hiyo na baadaye wataingia mkataba rasmi.
"Tumefanya mazungumzo na Supersports na tukakubaliana kwa kuanzia tu waoneshe mechi tano live kwa ajili ya majaribio, kwakuwa muda umeshakwenda na hawawezi kubadili ratiba ya vipindi vingine kwa muda mfupi," alisema Wambura.
Alizitaja mechi hizo ni ya Septemba 28 kati ya Azam FC na JKT Ruvu itakayochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Simba na Prisons itakayochezwa Septemba 29 Uwanja wa Taifa.
Mechi nyingine ni kati ya Yanga na African Lyon itakayopigwa Uwanja wa Taifa Septemba 30, Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar wataumana Azam Complex Oktoba Mosi na Simba na Yanga Oktoba 3 Uwanja wa Taifa.
Akizungumzia maslahi ya klabu kutokana na hatua hiyo ya jibu swali hukusu hatua hiyo na Supersports kuonesha alisema: "Tumeshakaa na klabu husika na kuwaeleza nia yetu ya kufanya hivyo na klabu zimeelewa, kwani ni fursa pekee kwao kujitangaza wachezaji wao na kucheza vizuri."
Alisema kituo hicho kitatumia gharama zake kuhakikisha kinarusha mechi hizo na kwa kufanya hivyo, katika mazungumzo yao yanayoendelea wana imani msimu ujao wataonesha karibu mecho zote za ligi hiyo.
Akizungumzia kuhusu mazungumzo ya mdhamini mkuu wa ligi hiyo, Wambura alisema amemsikia Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Warace Karia kwamba Kampuni ya Vodacom itaendelea kudhamini ligi hiyo na ndani ya wiki hii watasaini mkataba mpya.
Alisema bado wanakamilisha mambo ya msingi kama kujua mgawo wa klabu, haki za mdhamini pamoja na mambo mengine ambapo yatakapokamilika kila kitu kitawekwa wazi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment