11 September 2012

Simba, Azam 'mtoto hatumwi sokoni' leo


Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limesema mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Simba na Azam FC itapigwa leo kama ilivyopangwa saa 10.30 jioni baada ya maombi ya timu hizo ya kucheza usiku kukataliwa na serikali ambayo ndiyo mmiliki wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Hata hivyo mechi hiyo inatarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu kutokana na kila timu kujiandaa vyema na mechi hiyo, ambayo 'mtoto atakuwa hatumiwa sokoni'

Timu hizo juzi zilituma ombi hilo kwa nyakati tofauti ambapo Simba, ilitaka mechi hiyo ichezwe kuanzia saa 12 jioni na Azam ikaomba ianze saa moja usiku.

Akilitolea ufafanuzi suala hilo Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF Boniface Wambura, alisema ni kweli timu hizo ziliomba mechi ichezwe usiku lakini baada ya kuzungumza na serikali ikasema jambo hilo halitawezekana kwa sasa.

"Tumepokea ombi hilo jana (juzi) kwa njia ya e-mail kutoka kwa timu hizo, lakini tukakaa na serikali ambayo ndiyo mmiliki na haikuafiki ombi hilo kwa kuzingatia zaidi suala la usalama kwani miundombinu ni tatizo," alisema Wambura.

Alisema ni vigumu mechi hiyo kuchezwa usiku, hivyo mechi hiyo itabaki kama ilivyopangwa awali na tiketi zitauzwa leo uwanjani na kushauri mashabiki kununua tiketi mapema.

Wambura alisema kama walivyotangaza awali kwamba mechi hiyo ni kwa ajili ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara na pia asilimia 5 ya mapato, yatakayopatikana yatapelekwa hospitali ya Temeke kwa ajili ya huduma za kijamii.

Wakati huo huo, Ofisa Habari wa timu ya Azam, Jaffar Idd alisema kikosi chake kipo vizuri kwa ajili ya mechi hiyo na hawana majeruhi yeyote.

Alisema wameshinda mechi zote za kirafiki walizocheza na kwamba wana rekodi nzuri na Simba kwa siku za hivi karibuni, kwani wanapokutana nayo huibuka na ushindi hivyo watafanya juhudi kuhakikisha hilo linafanyika.

Naye Ofisa Habari wa timu ya Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mechi hiyo ni ya aina yake kutokana na ushindani ambao timu hizo kwa hivi sasa na kwamba watahakikisha wanawapa raha mashabiki wao.

Alisema kuwasili kwa mshambuliaji wao Emmanuel Okwi aliyekuwepo katika majukumu ya timu ya Taifa ya Uganda 'The Cranes', kutakifanya kikosi hicho kuimarika zaidi.

Kamwaga alisema kutokana na udhamini wanaoupata kwa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), watataka kuhakikisha wanatoka na ushindi ikiwa kama zawadi kwao.

Alisema ushindi huo pia utakuwa ni zawadi kwa TBL, ambayo hivi karibuni itawapa basi la kisasa kwa ajili ya kubeba wachezaji watakapokuwa wanakwenda kucheza mechi mbalimbali.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana katika robo fainali ya Kombe la Kagame mwaka huu na Azam iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 20,000 kwa Viti Maalumu A, Viti Maalumu B na C ni sh. 15,000, viti vya machungwa ni sh. 10,000 na viti vya bluu na kijani ni sh. 5,000.

No comments:

Post a Comment