11 September 2012

Bandari yainyuka Malindi 3-2


Na Mwajuma Juma, Zanzibar

TIMU ya Bandari juzi ilitoka kifua mbele, baada ya kuinyuka Malindi mabao 3-2 katika mechi ya Ligi Kuu ya Grand
Malt Zanzibar, iliyopigwa Uwanja wa Amaan mjini hapa.


Washindi walipata bao la
kwanza dakika ya 31, lililowekwa kimiani na Mussa Omar Kidishi.

Baada ya kufungwa bao hilo, Malindi iliamka usingizini na dakika moja kabla ya mapumziko ikasawazisha bao hilo kupitia kwa Amour Suleiman.

Kipindi cha pili Bandari iliingia kwa kwa nguvu na kufanya mashambulizi langoni mwa Malindi, ambapo dakika ya 57 ikaongeza bao la pili lililofungwa na Haisam Khamis.

Malindi ilisawazisha bao hilo, dakika ya 68 kupitia kwa Amour Suleiman.

Bandari ilijihakikishia ushindi dakika ya 78, baada ya Sharif Kitwana kuifungia timu hiyo bao la tatu.

Katika mechi nyingine iliyochezwa Uwanja wa Gombani mjini Pemba, Jamhuri iliinyuka Duma mabao 2-0 yaliyowekwa kimiani na Mfaume Shaaban dakika za 83 na 86 kwa mikwaju ya Penalti.

Ligi hiyo inatarajia kuendelea tena leo katika Uwanja wa Amaan, ambapo Chuoni na Mundu zitaoneshana ubabe.

No comments:

Post a Comment