11 September 2012

Yondan, Twite waitesa TFF


Na Elizabeth Mayemba

KAMATI ya Maadili, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilitarajia kupitia pingamizi la wachezaji 17 ambao usajili wao msimu 2012/2013 na utata, lakini majina ya mabeki Kelvin Yondan na Mbuyu Twite ndiyo yanayoonekana kuvuta hisia kubwa za wadau wa soka.

Awali kikao hicho kilitarajiwa kufanyika jana saa saba mchana, lakini kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF Boniface Wambura, kikao hicho kilisogezwa hadi saa 10 jioni baada ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Alex Mgongolwa kuwa na udhuru.

Kwa upande wa Yondan jina lake limewasilishwa na klabu mbili, kwanza Simba inayodai bado ina mkataba naye na wapinzani wao Yanga, waliomsajili kutoka kwa Wekundu hao wa Msimbazi ambapo walidai kuwa mchezaji huyo alikuwa huru.

Pia kwa upande wake Twite, Simba iliwasilisha malalamiko ya kufanyiwa mchezo usio wa kiungwana na Yanga kwa beki huyo.

Simba ilidai Twite alisaini mkataba na klabu hiyo Agosti Mosi, mwaka huu mbele ya viongozi wa Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) na APR na kulipwa dola za Marekani 30,000 na nyingine 2,000 za nauli ya kuja Dar es Salaam kujiunga na klabu hiyo, lakini mchezaji huyo akasaini Yanga.

No comments:

Post a Comment