24 September 2012
Shahidi ATCL akiri kuanda vocha magari chakavu
Na Rehema Mohamed
SHAHIDI wa kwanza katika ya kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia hasara Kampuni ya Air Tanzania Limited (ATCL) hasara ya Dola za Kimarekani 143,442.75 Bw.Ernest Kituli (54) ameilezea mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa yeye ndiyo aliyeandaa vocha za malipo ya magari chakavu 26.
Kesi hiyo inamkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mstaafu wa kampuni hiyo Bw.David Mattaka,ni Kaimu Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Bw.Elisaph Methuw na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Ndani, Bw.William Haji.
Shahidi huyo alieleza hayo mahakamani hapo jana alipokuwa akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Bi.Rita Tarimo huku akiongozwa na wakili wa serikali Bw.Shadrack Kimalo.
Alidai kuwa katika Kampuni ya ATCL yeye alikuwa Mhasimu kitengo cha Idara ya Malipo kama Msimamizi wa malipo kwa wafanyakazi wa ndani na wateja.
Alisema kuwa kati ya mwaka 2007 hadi 2008 alipokea maelekezo ya kuandaa vocha za malipo ya magari kutoka kwa mkuu wake wa kazi ambaye ni Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Bw.Elisaph Methuw.
Alidai kuwa siku hiyo aliandaa vocha sita za malipo ya magari hayo na kuzisaini na baada ya hapo alizipeleka kwa wakuu wake wa kazi ambao ni washtakiwa wa kesi hiyo.
Novemba 22 mwaka 2011,washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza wakikabiliwa na makosa sita ,ambayo ni kula njama kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka na walitenda kosa hilo kati ya Machi na Julai 2007.
Wanadaiwa kununua magari chakavu 26 bila kutangaza tenda ya ushindani na mkataba wa manunuzi wa magari hayo kutosainiwa na Mwanasheria mkuu wa Serikali.
Magari hayo waliyanunua kwa thamani ya dola za kimarekani 809,000 kutoka kampuni ya 3IN DALIMOUK MOTORS ya Dubai katika Jamhuri ya Emireti,bila ya kuwepo kumbukumbu ya manunuzi kinyume na kifungu cha 59 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2008 na kanuni zake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment