24 September 2012

Serikali yabaini utendaji mbovu bandarini Dar



Na Mraiam Mziwanda

SERIKALI imeendelea kubaini utendaji mbovu wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), katika kuhakikisha mradi wa boya la mafuta bandarini hapo unakamilika kwa wakati.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Bw. Charles Tizeba, aliyasema hayo Dar es salaam jana alipofanya ziara bandarini hapo ili kukagua maendeleo ya mradi huo.

Alisema nchi inapoteza fedha nyingi kutokana na boya hilo kutoanza kazi ambapo mbali na malalamiko waliyopokea kutoka kwa uongozi wa bandari wakimlalamikia mkandarais Bw. Leighton Offshore, ipo haja kukaa nae ili kumbaini anayechelewesha kazi hiyo.

“Hali si nzuri hapa bandarini, mbali ya ripoti tuliyoipokea kutoka kwa uongozi wa bandari wakimlalamikia mkandarasi, sisi tutawaweka pamoja ili kubaini ukweli na hatutakaa kimya, tutachukua hatua na kujua nani wa kuwajibishwa,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Bi. Sada Salum, alisema Serikali inakila sababu ya kuona boya hilo linakamilika kwa wakati kutokana na mapato yanayopotea bandarini hapo.

Alisema Serikali imefikia hatua ya kugharamia mradi huo kwa dola za Marekani milioni 70 ili kudhibiti mapato ambayo yanatokana na mfumuko wa bei ya mafuta.

“Gharama za maisha zinapanda kwa sababu ya mfumuko wa bei ambao chanzo chake ni upandaji wa gaharma za mafuta bandarini, hali hii inatokana na uwezo mdogo wa bandari yetu katika ushushaji mafuta kwani meli moja inachukua muda mrefu bandarini, kila siku moja ikikaa inalipa dola 20,000,” alisema.

Kaimu Meneja wa mamlaka hiyo, Bw. Madeni Kipande, alisema muda wa kulindana na kufanya kazi kwa mazoea bandarini hapo  umekwisha hivyo atahakikisha kila mmoja anawajibika.

“Watendaji wa TPA wanapaswa kuelewa kuwa Serikali iko macho, ulipaji gharama za kushusha mafuta ni kubwa, kila shilingi moja ni mbegu ya Serikali, wale waliozoea kupata ulaji kupitia miradi ya mamlaka hii wasahau bali wafanye kazi kwa uadilifu,” alisema.

Mradi wa ujenzi wa boya la mafuta yaliyosafishwa na yasiyosafishwa ulianza Aprili 2011 na ulitegemewa kukamilika Aprili mwaka huu ambapo fedha hizo zilitokana na mkopo kutoka Benki ya CRDB.

Lengo la boya hilo ni kuhakikisha meli zinapakua mafuta kwa muda mfupi ili kupunguza msongamano bandarini hapo.

No comments:

Post a Comment