28 September 2012

Serikali iungwe mkono kuondoa viatilifu




Na  Goodluck Hongo

KILIMO ni kati ya nguvu kazi inayoziwesha nchi nyingi zinazoendelea kujinasua na umaskini kwani wengi hukitegemea kama chanzo cha kipato.

Ili kumkomboa mtanzania katika umaskini, Tanzania ilianzisha sera la kilimo kwanza ikiwa ni pamoja na kuwapatia pembejeo za kilimo na kuwatafutia soko la uhakika.

Lengo kuu la serikali ni kuijenga Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, kwa kiasi kikubwa na kukua kwa sekta ya kilimo.

Njia bora za kuboresha kilimo nchini zitawawezesha wakulima wadogo wadogo kwa kushirikiana na vyama vya ushirika pamoja na wadau wengine kukubali kilimo kama ajira.

Licha ya changamoto zinazowakabili wakulima nchini wengi wao wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanapata pembejeo kwa wakati ili kuzalisha zaidi.

Serikali inajua kuwa pamoja na kuingiza matrekta kwa ajili ya kuwasaidia wakulima lakini pia kuna madawa ya kilimo ambayo yanaingizwa na mawakala wa kilimo ambapo baada ya muda yanageuka kuwa sumu na hatari kwa maisha ya binadamu.

Mfano halisi ni ule wa kilimo ndio uti wa mgongo badala ya msemo wa sasa wa kilimo kwanza kwani kuna watu ambao hutumia mianya hiyo kuingiza vitu vingi kwa kisingizio kama hicho lakini mwisho wa siku yanakuwa hayatumiki na kugeuka kuwa sumu.

Nionavyo, serikali lazima ichukue hatua kuangalia hata madawa ya kilimo na mifugo yanayoingizwa nchini kwani kwa nchi nyingi za Kiafrika hazina viwanda vya kuteketeza sumu ya madawa yaliyokwisha muda wake.

Nalazimika kusema hivi kwa sababu miaka mingi iliyopita kuliwahi kuingizwa kwa madawa mengi ya kilimo ikiwemo DDT ambapo baada ya kuingizwa kwa wingi yalikwisha muda wake na walioagiza waliyatelekeza kwa muda mrefu ambapo watu wengine wasio na uvumilivu waliamua kuvunja maghala na kuiba bila kujua kuwa yamekwisha muda wake.

Katika hili ni kwamba  asilimia kubwa ya madawa ya  kilimo ni ya maji na sio ya vidonge hivyo ni rahisi kuingia katika mkondo wa maji na kuingia chini ya ardhi na mwisho wa siku ni kuchoka kwa ardhi ambayo haiwezi kuzalisha kama awali.

Mfano halisi ulitokea Mkoani Morogoro hivi karibuni katika kituo cha garimoshi ambapo kulikuwa na maghala ambayo yalihifadhiwa madawa hayo lakini watu wasiojulikana walitoboa mabati na kuyatoa baadhi ya madumu ambayo yalihifadhi sumu hiyo yalikaa kwa muda mrefu yakiwa nje huku mvua zikinyesha na kusafirisha sumu hiyo katika eneo lingine.

Binafsi niliyashuhudia madumu hayo yakiwa yametupwa nje bila kuwa na mwenyewe  lakini baada ya kueleweshwa na mtaalamu aliyekuwepo.

Ingawa sumu hiyo ipo kwa kisasi kikubwa lakini katika bara la Afrika hakuna kiwanda cha kuteketeza sumu hiyo ambapo lazima ichukuliwe na kupelekwa nje ya nchi ili kuiangamiza sumu hiyo ambapo katika bara la Afrika nchi nyingi zimeathirika.

Nionavyo vyema serikali ikaangalia kwa umakini madawa ya kilimo ambayo yanaingizwa nchini kwani asilimia kubwa ya watanzania hutegemea kilimo.

Ili kunusuru hekta milioni 5.1 zinazolimwa nchini kila mwaka serikali inatakiwa kuchukua hatua ya kudhibiti uingizwaji holela wa madawa ya kuulia viatilifu.

Sehemu kubwa ya ardhi ikipata madhara kutokana na sumu hii Taifa litapoteza pato kwa asilimia kubwa kwani kuanzia mwaka 1985, mazao ya chakula yaliongezeka kwa asilimia 3.5, na mazao ya biashara kwa asilimia 5.4.   

Ni wakati sasa wa kumaliza dawa za kilimo zilizokwisha muda wake pamoja na kunusuru uharibifu wa mazingira kote nchini na kukifanya kilimo kuwa kimbilio la wengi.

0689 444464

No comments:

Post a Comment