28 September 2012

Mkutano wa AGRA uwe na manufaa kwa wakulima wetu



RAIS Jakaya Kikwete, juzi alifungua mkutano wa Mapinduzi ya Kijani katika Afrika (AGRA), jijini Arusha ambao unajadili suala zima la mageuzi ya kilimo katika nchi mbalimbali za Afrika.

Mkutano wa kwanza kama huo ulifanyika nchini Ghana miaka miwili iliyopita.

Katika mazungumzo yake na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mapinduzi AGRA, Bw. Kofi Annan, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa zamaniwa Umoja wa Mataifa (UN), Rais Kikwete alisema huwezi kuzungumzia maendeleo ya kilimo katika Afrika bila kumshirikisha mkulima mdogo.

Aliongeza kuwa, Afrika haiwezi kupata maendeleo makubwa bila kumwezesha mkulima mdogo ambaye anakabiliwa na changamoto nyingi ambazo peke yake hawezi kupambana nazo.

Rais Kikwete alisema mkulima mdogo katika nchi nyingi za Afrika ameendelea kutumia zana za jadi kama jembe la mkono ambalo haliwezi kumsaidia apige hatua ya maendeleo kutokana na changamoto alizonazo.

Haya ni maneno mazito ambayo ameyasema Rais Kikwete katika mazungumzo yake na Bw. Annan, wakati Tanzania ikiendelea kutekeleza mpango mkakati wa 'Kilimo Kwanza'.

Neno ‘Kilimo Kwanza’ ni kauli mbiu ambayo inawahamasisha wakulima nchini kuongeza juhudi kwenye kilimo cha kisasa ili uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara uweze kukua.

Serikali ya Rais Kikwete imedhamiria kuleta mapinduzi ya kijani katika sekta hiyo kiuchumi na kijamii lakini tangu kuanza kwa mpango huo, zipo kasoro nyingi zilizojitokeza.

Kasoro hizo zinahitaji kutatuliwa mapema ili tusipoteza maana halisi na kushindwa kuleta mapinduzi yanayokusudiwa kwa mkulima.

Baadhi ya wadau wa kilimo, wamekuwa wakionesha wasiwasi wa kufanikiwa kwa mpango huo na kuleta mapinduzi ambayo yanakusudiwa kutokana na kasoro zilizopo.

Wadau wa kilimo wanasema,  bila kusikiliza matatizo waliyonayo wakulima wadogo na kuyapatia ufumbuzi wa haraka, mafanikio yanayotarajiwa katika sekta hii hayawezi kufikiwa.

Sisi tunasema kuwa, Tanzania bado ina safari ndefu ili kufanikisha mpango huo. Lengo la Serikali ni zuli lakini vikwazo ni vingi.

Yawezekana mpango wa Kilimo Kwanza upo kisiasa zaidi, tatizo kubwa linaloweza kuufanya ukakwama ni ukosefu wa miundombinu ambayo ni pamoja na barabara hasa ziendazo vijijini kwenye mazao ambazo hazipitiki kirahisi.

Hali hiyo inachangia pembejeo zishindwe kufika sokoni kwa wakati, baadhi ya viongozi serikalini na wataalamu wa kilimo kushindwa kuwafikia wakulima vijijini na kuwapa elimu ya kilimo cha kisasa jambo linalochangia malengo ya mpango huo kukwama.

Kukosekana kwa soko la uhakika la mazao ya wakulima, huchangia mazao mengi kuharibika kabla ya kufika sokoni ili mkulima apate faida badala yake huingia hasara.

Wakulima wengi wadogo hawafahamu mbinu za kilimo cha kisasa, uvunaji na uhifadhi wa mazao yao kabla ya kufikishwa sokono.

Imani yetu ni kwamba, ili mkulima apate mazao yenye kukubalika kwenye soko, wataalamu wa kilimo wanapaswa kuwa karibu na wakulima badala ya kukaa ofisini kama wanavyofanya sasa.

Upo umuhimu wa Serikali kuwafikia wakulima wadogo katika maeneo yao ili kusikiliza matatizo waliyonayo na ushauri ambao utatolewa katika mkutano huo, ufanyiwe kazi kwa maendeleo ya wakulima na Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment