24 September 2012
...Timua timua yamkumba Tom Saintfiet, 'ulevi' wamponza
Na Elizabeth Mayemba
KIMENUKA Yanga! Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo imemtimua Kocha Mkuu wake, Mbelgiji Tom Saintfiet kwa madai kwamba anaupungufu mwingi na kubwa zaidi ni baada ya mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Prisons, ambayo walitoka suluhu ambapo kocha huyo na wachezaji wakaenda kukesha baa hadi asubuhi.
Baada ya kocha huyo kusitishiwa kibarua chake rasmi jana, sasa hivi timu hiyo itakuwa chini ya msaidizi wake, Fredy Felix Minziro hadi atakapoletwa kocha mwingine.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Clement Sanga, alisema matokeo mabaya ndiyo yamefanya Saintfiet asitishiwe mkataba pamoja na mambo mengine.
“Kuna upugufu mwingi mno kwa huyu kocha, kwani hata timu ilipokwenda Mbeya na kutoa sare na Prisons alilalamikia huduma, lakini sisi taarifa tulizozipata ni kwamba alikwenda kulewa na wachezaji, sasa jambo kama hilo sisi hatuwezi kulifumbia macho," alisema Sanga
Alisema kuna upungufu mwingine mwingi, ambao hawawezi kuusema hadharani, lakini ni mengi akitolea mfano timu ilipotoka Mbeya, uongozi ulitaka timu iende moja kwa moja Morogoro, lakini yeye akalazimisha irudi Dar es Salaam, tena iende Morogoro.
"Kwa hali ya timu zetu za Tanzania kwanza ni gharama, lakini alikuwa mbishi, sasa hali kama hiyo wachezaji lazima wachoke na ndiyo maana tukafungwa na Mtibwa Sugar mabao 3-0," alisema.
Sanga alisema timu iliporudi kutoka Morogoro, wakaamua iingie kambini, lakini yeye akapinga na kudai kuwa timu kubwa kama Barcelona huko Ulaya, hazikai kambini, hivyo yeye anataka watumie mfumo wa Ulaya kitu ambacho wakaona watashindwana naye hapo baadaye.
Saintfiet aliichukua Yanga Julai mwaka huu, akirithi mikoba ya Mserbia Kostadin Papic, ambapo kipindi chote ameiongoza timu hiyo kucheza mechi 14. Pia aliiwezesha timu hiyo kutwaa kombe la Kagame.
Uongozi huo pia umemtangaza Lawrence Mwalusako kurithi mikoba ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Selestine Mwesiga na Dennis Oundo kuwa kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, huku nafasi ya Sendeu ikiachwa wazi mpaka watakapopata mwingine.
Sanga alisema uongozi haukurudhishwa na utendaji mzima wa Sekretarieti ya klabu hiyo, wengine waliokumbwa na panga hilo ni Masoud Saad, aliyekuwa Ofisa Utawala, Philip Chifuka aliyekuwa Mhasibu na Hafidh Saleh aliyekuwa Meneja ambaye anahamishiwa kwenye majukumu mengine.
Mbali na Mwalusako na Oundo, kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Sekilojo Chambua anatajwa kupewa nafasi ya umeneja.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment