10 September 2012

Saintfeit roho kwatu kwa Kavumbagu



Na Zahoro Mlanzi

KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga, Tom Saintfeit ameridhishwa na kiwango kilichooneshwa na mshambuliaji wake mpya raia wa Burundi, Didier Kavumbagu wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Moro United iliyopigwa juzi Uwanja wa Bora, Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo, Kavumbagu aliifungia timu yake mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-0 huku mabao mengine yakifungwa na Shamte Ally na Juma Abdul.

Akizungumza na gazeti hili mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo juzi, Saintfeit alisema mechi hiyo aliomba ichezwe kwenye uwanja huo kutokana na mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Prisons ya Mbeya itapigwa kwenye uwanja kama huo.

"Niliambiwa na viongozi wangu kwamba tutacheza mechi ya kwanza ugenini jijini Mbeya dhidi ya Prisons ambapo uwanja wao wa Sokoine unafanana na huu tuliochezea, hivyo wachezaji wangu inawabidi wazohee mazingira ya aina yoyote," alisema Saintfeit.

Alisema licha ya kuchezea kwenye uwanja huo lakini amefurahishwa na uwezo wa ufungaji uliooneshwa na Kavumbagu ambapo alidai sasa safu yake ya ushambuliaji imekamilika na itakuwa na ushindani mkubwa.

Alisema awali alikuwa akimtegemea Said Bahanunzi na Jeryson Tegete lakini ujio wa mshambuliaji huo ni dhahiri sasa kila mmoja atajituma ili apate namba katika kikosi cha kwanza.

Alisema kwa mujibu wa uongozi wake, wataondoka jijini Dar es Salaam Jumatano kwenda Mbeya kwa ajili ya mchezo huo na kuwatahadharisha nyota wake kwamba kila mechi katika ligi hiyo ni ngumu hivyo wasipoteze hata mechi moja.

Hiyo ni mechi ya 13 kwa kocha huyo kucheza huku akishinda mechi 12 na kupoteza moja tangu alipokabidhiwa mikoba ya kuinoa timu hiyo wiki chache kabla ya kuanza michuano ya Kombe la Kagame ambapo alilitwaa.

No comments:

Post a Comment