10 September 2012

Ngao ya Jamii Kesho ------------------------ Simba, Azam zatunishiana 'msuli' *Macho yote leo Yondani, Twite


Na Zahoro Mlanzi

WAKATI  mabingwa wa Ligi Kuu Bara, timu ya Simba na washindi wa pili, Azam FC wakikitambiana kila moja kufanya vizuri katika mechi ya kesho ya Ngao ya Jamii, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi kwa Wachezaji ya Ligi Kuu Bara, leo itakata mzizi wa fitina  juu ya suala la Kelvin Yondani na Mbuyu Twite baada ya Simba na Yanga kutofikia muafaka.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti Dar es Salaam jana, Maofisa Habari wa timu hizo, Ezekiel Kamwaga (Simba) na Jaffar Idd (Azam), walisema timu zao zimejiandaa vizuri kwa mechi hiyo na kinachosubiliwa ni siku ya tukio ifike.

Kwa upande wa Kamwaga alisema hivi sasa timu yao imekamilika hasa baada ya kucheza mechi nyingi za kirafiki zilizomsaidia Kocha Milovan Cirkovic kupata kikosi chake cha kwanza atakachokitumia katika ligi kuu.

"Tunajua wana-Simba wana wasiwasi na kikosi chao lakini tungependa kuwajulisha kwamba, klabu imefanya usajili wa nguvu na matokeo mabaya waliyoyapata ni kutokana na kocha wetu kutaka kupata kikosi cha kwanza ambacho tayari ameshakipata," alisema Kamwaga.

Alisema hivi karibuni walifungwa na SOFAPAKA ya Kenya kwa mabao 3-0 katika mchezo ambao Milovan aliamua kuchezesha wachezaji wote ili kuangalia uwezo wa kila mchezaji na hilo kiufundi limefanikiwa na sasa hana wasiwasi na kikosi chake.

Aliwaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi katika mechi hiyo ambayo ndio itakayowapa taswira halisi ya ubora wa kikosi chao katika kuelekea ligi kuu na kwamba hasira za SOFAPAKA zitaishia kwa wapinzani hao.

Wakati huohuo, Kamwaga aliongeza kwamba klabu yao ilisoma dua ya kuwaombea wanachama, wapenzi, wachezaji, viongozi na mashabiki wao waliofariki dunia ambapo lilifanyikia Makao Makuu ya klabu hiyo, Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini na kutumia saa sita.

Alisema huo ni utamaduni wa klabu yao kufanya hivyo kabla ya kuanza kwa ligi ambapo huwakumbuka watu mbalimbali waliotoa mchango mkubwa katika kufanikisha maendeleo ya timu hiyo.

Alisema dua hilo liliongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum.

Naye Idd alisema hawaihofii Simba kwani ni timu kama zilivyo timu zingine nchini na kwamba kikubwa watakachohakikisha ni kutwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza na kuandika historia nyingine.

Alisema walifika fainali ya Kombe la Kagame kitu ambacho kwa timu yao ni mafanikio makubwa, hivyo wakitwaa na kombe hilo watazidi kujitangaza zaidi na kwamba katika michuano ya Kagame, waliifunga Simba mabao 3-1.

Alisema kocha wao, Bunjak Boris amezidi kukiimarisha kikosi chao ukilinganisha na kilivyokuwa katika michuano ya Kagame kwa kubadili programu ya mazoezi, hivyo amewaomba mashabiki wao kujitokeza kuishangilia timu hiyo.

Katika hatua nyingine, Kamati ya Sheria iliyo chini ya Mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa leo inatarajia kukutana kumalizia rufani mbalimbali zilizowasilishwa mbele ya kamati yake kuhusu usajili wa baadhi ya wachezaji mbalimbali wa ligi kuu.

Miongoni mwa wachezaji hao ni mabeki wa Yanga, Kelvin Yondani na Mbuyu Twite, mchezaji wa Simba, Ramadhani Chombo 'Redondo' ambao ndio gumzo katika kikao hicho kinachotarajiwa kufanyika leo endapo kolamu ya wajumbe itatimia.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti hili ilizipata wakati linakwenda mitamboni ni kwamba viongozi wa Simba na Yanga, wameshindwa kuafikiana baada ya Simba kutaka ilipwe zaidi ya sh. milioni 60 na Yanga kukataa kulipa fedha hizo.

No comments:

Post a Comment