05 September 2012
Guninita amtaka Madabida, Katibu wake wajieleze
Na Heri Shaaban
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam kimeiagiza Kamati ya Maadili ya CCM Mkoa huo, kuwaita na kuwahoji Mwenyekiti, Bi.Zalina Madabida na Katibu wake, Bi.Tatu Malihega (UWT) Dar es Salaam kwa kukiuka kanuni na sheria za chama kwa kuzuia chaguzi za Jumuiya za CCM Wilaya ya Kinondoni zisifanyike.
Tamko la kuwaita viongozi hao wahojiwe na Kamati ya Maadili CCM lilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa, Bw.John Guninita wakati wakizungumza na waandishi wa habari.
Bw.Guninita alisema Agosti 29, mwaka huu chama hicho kilifanya uchaguzi wa Jumuiya zote, lakini Umoja wa Wanawake wa Wilaya hiyo, uchaguzi haukufanyika baada ya Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Mkoa wa Dar es Salaam, Bi.Zalina Madabida na Katibu wake Bi.Tatu Malihega kuweka pingamizi.
"Naagiza kamati ya maadili kuwaita na kuwahoji Mwenyekiti wa UWT, Bi.Zalina Madabida na Katibu Bi.Tatu Malihega kutokana na kukiuka taratibu za chama ili chama kiweze kutoa adhabu kali iwe fundisho kwa viongozi wengine," alisema Bw.Guninita.
Alisema kuwa ameshangazwa na viongozi hao wa UWT kuingilia maamuzi ya kuzuia chaguzi za jumuiya, wakati wao hawana maamuzi yoyote ndani ya CCM.
Aliwaagiza Bi.Madabida na Malihega kuhakikisha uchaguzi huo waliozuia unafanyika kama ulivyopangwa, Pia wasiingilie taratibu za chama, kwani chama hakiwezi kuzuiwa na mtu mmoja kufanya jambo lake.
"Maagizo ya Halmashauri Kuu hayakutekelezwa kutokana na viongozi hao kukiuka sheria za chama, Katiba za CCM na kukwamisha mipango ndani ya chama hiki, naachia kamati hiyo iweze kuwahoji na kuwapa adhabu," alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment