17 September 2012

Pingamizi za Lulu zaanza kusikilizwa leo



Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Rufaa leo inatarajiwa kuanza kusikiliza pingamizi za kuchunguza umri wa msanii maarufu wa filamu, Elizabeth Michael 'Lulu'.
Maombi hayo yatasikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo, ambao ni Jaji Benard Luanda, Jaji January Msoffe na Jaji Katherine Oriyo.


Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,ambapo anadaiwa kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba Aprili 7, mwaka huu, Sinza Vatican, Dar es Salaam.

Umri wa msanii huyo umezua utata baada ya mawakili wanaomtetea, kudai kuwa ana miaka 17 na si 18 kama hati ya mashtaka inavyoonesha na kuomba kesi yake isikilizwe katika Mahakama ya Watoto.

Mahakama Kuu ilikubali kuchunguza umri wa mshitakiwa huyo, lakini siku iliyotarajia kuanza kufanya uchunguzi wa umri halali wa mshtakiwa, upande wa mashtaka uliitarifu mahakama hiyo kuwa umewasilisha Mahakama ya Rufani maombi ya marejeo ya uamuzi huo.

Jaji Fauz Twaib ndiye aliyetoa uamuzi wa kukubali kuchunguza umri huo, lakini kutokana na upande wa mashtaka kuwasilisha maombi yao mahakama ya rufani aliahirisha kuendelea na uchunguzi wa umri wa msanii huyo hadi Mahakama ya Rufaa itakapotoa uwamuzi wake.

Vielelezo vya upande wa utetezi vinaonesha kuwa mshtakiwa huyo ana umri wa miaka 17, huku  vielelezo vya upande wa mashtaka navyo vinaonesha kuwa mshtakiwa huyo ana umri wa zaidi ya miaka 18.

Baadhi ya vielelezo vilivyowasilishwa na upande wa mashtaka kuthibitisha kuwa mshtakiwa ana umri wa zaidi ya miaka 17 ni pamoja na hati ya kusafiria na leseni ya kuendesha gari.

Vielelezo vya upande wa utetezi ni  pamoja na viapo vyote vya wazazi wa mshtakiwa, cheti cha kuzaliwa na cha ubatizo vya mshtakiwa ambavyo vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo alizaliwa Aprili 16, 1995, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kupewa cheti cha kuzaliwa namba B.0318479 cha Julai 23, 2004.

No comments:

Post a Comment