11 September 2012

Moto waunguza mabweni Bunda



Na Raphael Okello, Bunda

MOTO mkubwa umezuka na kuteketeza mabweni mawili ya wanafunzi zaidi ya 100 katika Shule ya Sekondari Ikizu, iliyopo Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, inayomilikiwa na Kanisa la Waadventista Wasabato.

Hakuna mwanafunzi aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa katika ajali hiyo licha ya moto huo kuunguza magodoro, vitanda, nguo za wanafunzi pamoja na vifaa mbalimbali.

Ajali hiyo ilitokea mwishoni mwa wiki saa tatu usiku wanafunzi wakiwa madarasani na kuzimwa saa sita.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Joshua Mirumbe, alisema moto huo ulizimwa na timu ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa kushirikiana na Kikosi cha Uokoaji kutoka mjini Musoma.

Alisema chanzo cha moto huo hakijajulikana hivyo wameunda tume ili kufanya kazi hiyo na kutoa tathmini ya hasara iliyojitokeza.

Alisema wanafunzi hao ambao ni wa kidato cha kwanza, pili na tatu hawatarudi nyumbani bali wataendelea na masomo pamoja na kuwataka wazazi, walezi, marafiki na mashirika mbalimbali kuwapa msaada wanafunzi hao.

No comments:

Post a Comment