11 September 2012

14 mbaroni kwa kuvunja kontena bandarini


Jessica Kileo na Leah Daud

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linawashikilia watu 14 kwa tuhuma za jaribio la kuvunja kontena bandarini, kuiba vipande 19 vya madini ya shaba, mafuta ya petroli lita 360 na dizeli lita 60.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema tukio hilo lilitokea Septemba 8 mwaka huu, saa nane usiku katika shedi namba saba.

Alisema askari wa zamu kitengo cha kontena walisikia kishindo cha vitu vizito vikitumbukizwa ndani ya behewa tupu namba 014NB-MCM129 ndipo walipotoa taarifa Kituo cha Polisi.

Aliongeza kuwa, polisi na askari msaidizi wa bandari walianza kufuatilia na kufika eneo la tukio linalohifadhi makasha ya madini kwenye kituo cha treni cha Tazara namba DHI 2006.

“Askari walipofika eneo hilo, walifanikiwa kuwakamata watu 10 ambao ni Bw .Charles Rejina (49), fundi cherehani mkazi wa Tandika Azimio, Bw. Range Boaz (40), fundi pancha mkazi wa Kichemuchemu Mbagala na wenzao nane,” alisema.

Alisema mbinu iliyotumiwa na watuhumiwa hao ni dereva wa treni  Bw. Abhrahamu Shebe, ambaye aliingiza kichwa cha treni namba DHI 2006 bandarini akiwa na Bw. Bakari Chitanda.

Ilidai baada ya kufika eneo la Tambukalei Tandika, walisimamiwa kichwa cha treni, kupakia watu nane na kwenda nao bandarini.

“Kawaida kichwa cha treni kuingia bandarini na askari, polisi msaidizi wa mamlaka ya bandari aliyekuwa zamu aliwafungulia na kuingia, watu hao walishuka mbele na kuanza kuingurumisha treni ili sauti isisikike wakati vipande hivyo vikipakuliwa,” alisema.

No comments:

Post a Comment