24 September 2012
Mkutano wa kuweka sera ya kudhibiti ulevi kufanyika leo
Na Mwandishi Wetu
MKUTANO wa Kimataifa ambao utajadili umuhimu wa nchi za Afrika Mashariki kuwa na sera ya kudhibiti ulevi, unatarajiwa kuanza leo mjini Arusha.
Mkutano huo wa siku mbili, utashirikisha washiriki 80 ambao kazi zao zinaguswa na madhara ya ulevi ukiwa na kauli mbiu inayosema
“Ulevi ni matatizo chukua hatua sasa”.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini (TAMWA), Bi. Ananilea Nkya, alisema mkutano huo utafunguliwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hussein Mwinyi.
Alisema Balozi wa Sweden nchini, Dkt. Lennrth Hjelmaker, atatoa mada kuu kuhusu madhara ya ulevi na umuhimu wa kuwa na sera ambayo itadhibiti matumizi mabaya ya pombe.
“Ulevi una madhara makubwa kwa jamii sambamba na kuchochea migogoro majumbani na kusababisha ajali ambazo zinaua na wengine kupata ulemavu wa maisha,” alisema.
Aliongeza kuwa, washiriki wa mkutano huo wanatoka nchi za Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Malawi, Sweden, Norway na wenyeji Tanzania.
Bi. Nkya alisema mada ambazo zitawasilishwa katika mkutano huo ni pamoja na zile ambazo zitajadili hatua zilizofikiwa na nchi za Afrika Mashariki kuweka sera ya kudhibiti vilevi.
Alisema mwakilishi kutoka nchini Malawi ambaye nchi yake imechukua hatua ya kutunga sera ya kudhibiti ulevi, atawasilisha mada kuzungumzia fursa na changamoto zake.
Aliongeza kuwa, siku ya pili kutakuwa na warsha nne ambazo zitazungumzia mada mbalimbali zote zikilenga kuelimisha na kuhamasisha washiriki kuona umuhimu wa nchi hizo kuwa na sera ya kudhibiti ulevi.
“Mkutano huo umeandaliwa na Shirika la Kimataifa lisilokuwa la Kiserikali IOGT, ambalo linahamasisha maendeleo kwa kushirikiana na mashirika mengine ya kijamii Afrika Mashariki.
“Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani nchini Dkt. Neema Kileo na mwakilishi IOGT, ngazi ya kimataifa Kristina Sperkova, watatoa ujumbe maalumu katika mkutano huu,” alisema Bi. Nkya.
Mkutano huo utafungwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Richard Sezibera.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment