10 September 2012

Mkaguzi jela miaka miwili kwa ufisadi Muheza



Na Benedict Kaguo, Muheza

MKAGUZI wa ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga, Bw. Nducha Jairos (40), amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia kwenye makosa 20 yaliyohusu matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa fedha.

Bw. Jairos alitiwa hatiani katika Mahakama ya Wilaya hicho na Hakimu Mfawidhi Salum Msingiti, ambapo kesi hiyo ilifunguliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Kaimu Mkuu wa TAKUKURU, mkoani hapa, Bw. Sadiki Nombo, alisema mshtakiwa alifikishwa mahakamani Julai 13,2011 baada ya shauri lake kusomwa Machi 25,2011 bila kuwepo mahakamani.

Alisema mshtakiwa alikuwa akikusanya fedha kutoka kwa watendaji wa vijiji ili kuwanunulia vitabu vya kutunza kumbukumbu za mahesabu bila kuwapatia stakabadhi.

Bw. Nombo alisema mshtakiwa pia hakukabidhi vitabu husika kwa watendaji hao kama alivyodai badala yake alitumia fedha hizo kujinufaisha mwenyewe.

“Mshtakiwa amehukumiwa kifungo hiki baada ya kushindwa kulipa faini ya sh. milioni 11, au kwenda jela miaka miwili,” alisema.

Hata hivyo, taasisi hiyo imetoa wito kwa wananchi wote hasa watumishi wa umma, kuzingatia maadili, kutojihusisha na vitendo vya rushwa.

1 comment:

  1. Hata kama amefanya kosa hilo akafungwa haina tija yoyote katika kupambana na ufisadi uliokubuhu.Kama mapapa ya ufisadi yanatamba barabarani na yameachwa bila kufanywa chochote, huyo si ameonewa tu?

    ReplyDelete