24 September 2012

'Mfumo OMR ukitumika vizuri utapunguza udanganyifu'



Na Zourha Malisa

NI wazi wakati umefika tufikirie sana juu ya swala la elimu,mpango wa elimu Tanzania umewekwa kwa sababu gani na shabaha yake ni nini.


Tutakapoamua kutazama hilo tutatazama kama muundo wa elimu inayopatikana nchini inafaa kwa kazi inayotakiwa kufanya,na kutoka na uchunguzi huo tunaweza kufikiri kama kwa hali yetu ya leo tunaweza kufanya mabadiliko zaidi au kama kunahaja ya kufanya mapinduzi katika mpango mzima wa elimu.

Tutakapo fahamu aina ya Taifa tunalotaka kujenga ndipo tutakapoweza kuweka mipango ya elimu yenye kutufikisha kwenye shabaha hiyo.

Na si kuweka mipango mepesi ya elimu ya kuweza kuzidi kudumaza elimu yetu na kwa watoto wanaotegemea elimu hiyo kuwa mkombozi wao.

Mipango ya elimu isiwe kwa kujenga shule nyingi za kata huku kukiwa na uhaba wa walimu, vifaa vya kufundishia, viwanja vya michezo.

Ingawa vijana hao wanaopata nafasi ya kuingia katika shule za sekondari idadi imeongezeka kwa kiwango cha ufaulu kuongezeka,huku idadi ya wasiojua kusoma na kuandika kuongezeka kwa kasi.

Ili kuthibiti wizi wa mitihani kwa watahiniwa serikali imeanzisha mfumo mpya wa kujibu mtihani hususani wa darasa la saba unaotumia teknolojia mpya ya Optical Mark Reader (OMR) ambapo watahiniwa watatumia fomu maalum za OMR kujibia mtihani na majibu yatasahihishwa kwa kutumia kompyuta.

Mtahiniwa atatakiwa kuweka alama ya mstari au kusiliba kwenye kisanduku chenye jibu analoona ni sahihi katika machaguo matano aliyopewa
Mfumo huu unalenga kuinua kiwango cha ufaulu nchini.

Pamoja na kuzibiti udanganyifu ambao ulikuwa unafanywa na baadhi ya wanafunzi, kutokana na udanganyifu huo kunasababisha kuwepo na ufaulu mkubwa huku wasiojua kusoma na kuandika idadi inazidi kuongezeka kila mwaka.

Baadhi ya shule zimeonekana zikifaulisha wanafunzi kwa kiwango cha hali ya juu ingawa hao waliofaulu hawajui kusoma wala kuandika tatizo linaenda kwa walimu wa sekondari ambao wanaanza kufanya kazi ya ualimu wa shule za awali kuwafundisha kusoma na kuandika wanafunzi ambao wamefaulu darasa la saba.

Serikali kupitia wizara yake ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetoa onyo kali kwa walimu na watendaji wengine kujihusisha na vitendo vya udanganyifu kwenye mtihani wa darasa la saba wakati huo mfumo mpya wa kujibu maswali umeanza kutumika.

Mbali na kutoa onyo kali pia Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Bw. Philipo Mulugo alizitaka shule binafsi ambazo walimu wake walihusika na udanganyifu wakati wa mtihani uliopita wachukuliwe hatua.

Hali hii itasababisha hata walimu waliokuwa na nia ya kufanya hivyo kuogopa kwani wakiamini kuwa watakapo gundulika udanganyifu unaofanywa sheria itachukua mkondo wake kwa kuwajibisha walimu hao.

Mfumo huu mpya wa kujibu mtihani kwa fomu maalum za OMR zitasaidia kupunguza udanganyifu kwa hali kubwa kwa upande wa wanafunzi pamoja na baadhi ya walimu wenye mtindo huo wa kuvujisha mitihani.

Serikali inania nzuri ya kuanzisha mfumo huo ili kukomesha tabia ya wizi wa mitihani kwa baadhi ya walimu pamoja na udanganyifu uliokuwa unafanywa na baadhi ya wanafunzi hili ili kuboresha elimu na kuinua kiwango cha elimu katika nchi yetu.

Udanganyifu katika swala la mitihani ni pana sana na kwa njia hii ya mfumo huo mpya serikali itatimiza lengo lake kwa kuzibiti tabia hiyo ili lengo litimie la kuwa na elimu bora kwa Taifa letu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Ualimu (DUCE), Bw. Ruben Ndimbo anasema kuwa suala la udanganyifu ni dhana pana ambalo si la kuliangalia kwa juu juu inatakiwa kuanagalia chanzo cha udanganyifu huo hususani katika ngazi ya elimu ya msingi.

Bw.Ndimbo anasema kuwa suala la udanganyifu linachangiwa na kiasi kukubwa na usimamizi mbovu pamoja na mmomonyoko wa maadili ya kazi, kwa baadhi ya walimu wa shule za msingi.

Anasema kuwa mmomonyoko wa maadili ya kazi kwa baadhi ya walimu inachangia walimu kutojua wajibu wao kwenye masuala yote ya kufundisha hadi usimamizi wa mitihani yao hivyo kunaulazima wa kutafuta sababu  kwanza kwa nini usimamizi ni mbovu.

Kwa mujibu wa Bw.Ndimbo anasema kuwa anapatwa na wasiwasi kuwa walimu wanatumia usimamizi mbovu kama kitega uchumi chao.

“Wanatumia kama kigezo chao cha kuongezea mapato baada ya serikali kusuasua katika kuwaboreshea kipato chao na mazingira yao kiujumla,“ anasema

Bw.Ndimbo anaongezea kuwa mfumo huo mpya wa OMR ndio unaweza ukaongeza wizi kwa kuwa hata asiyejua kusoma na kuandika ataweza kujibu mtihani huo kwa kuweka kivuri sehemu kwenye kisanduku anachoamini ndicho chenye jibu sahihi hata kwa kumchungulia mwenzie

Anasema kuwa mfumo huo si jibu la kuondoa tatizo la udanganyifu kwenye mtihani ila serikali ichukue hatu ya kutoa mafunzo ya maadili ya kazi kwa walimu ili waweze kutambua wajibu wao kwa Taifa.

Pamoja na hayo kuboresha mazingira ya walimu hususani nyumba wanazoishi ziwe na tija ili waweze kutimiza wajibu wao.

Wajibu wao ni pamoja na kusimamia mitihani kimaadili pasipo kuweka hali yoyote ile ya udanganyifu kwa lengo la kutaka kufaulisha wanafunzi kwa kiwango cha juu.

Nia ya serikali itafanikiwa ukilinganisha na mazingira yaliyopo katika shule zetu, kwani mfumo huo mpya unahitaji usafi wa hali ya juu kwani majibu yatasahihishwa kwa kutumia komputa.

Jambo jipya linapoazishwa huwa kunakuwa na mategemeo tofauti tofauti kwa wanachi na lazima kuwe na mazingira yaliyoandaliwa kwa ajili ya kuweza kupambana na jambo hilo jipya.

Bw. Moses Kyando ambaye yeye ni mwanafunzi wa Chuo kikuu Huria anasema kuwa kila kitu kina changamoto yake hasa kinapokuwa kipya na kwa vyovyote upya wake unaweza kuwa na matokeo chanya kwenye ufaulu wa watoto.

Bw. Kyando anasema kuwa serikali kupitia wizara yake imejitahidi mfumo huo kufanyiwa majaribio ya kutosha kwa kila mwanafunzi wa darasa la saba.

“Mfumo umekwisha fanyiwa majaribio ya kutosha na karibu kila mwanafunzi anayefanya mtihani leo hii (ukiacha watoro) amefanyia mazoezi zaidi ya mara mbili kujiandaa na matumizi ya OMR.” Anasema Kyando

Walimu wamejitahidi kuwapa wanafunzi mafunzo ya kujibu mtihani huo si zaidi ya mara mbili kwa kila mwanafunzi aliyehudhuria darasani ili kuhakikisha wanaweza kujibu vizuri ili kuinua kiwango cha elimu

Anasema kuwa Kwa hivyo shida siyo mfumo wa OMR shida ni watu kubadili mtazamo kwa kile wanachokiamini na kuukubali mfumo mpya inayolenga kuongeza uwezo wa kufaulu wa mwanafunzi binafsi na kukomesha undanganyifu wa mtihani.

Pia walimu wanatakiwa kujua wajibu wao na kuacha kuangalia maslahi yao binafsi huku wakijenga Taifa la watu wasiojua kusoma na kuandika kwa kutofanikisha wajibu wao wa ufundishaji unaolenga kuinua kiwango cha elimu.

Bw.Kyando anasema kuwa mfumo huu unakumbwa na changamoto kubwa hasa kwa shule za vijijini ambazo hazina miundo mbinu rafiki na mfumo huo hivyo kusababisha ugumu kwa wanafunzi katika utumiaji wa huo mfumo.

“Huko kijijini ndiko kunachangamoto kubwa hasa kwa shule ambazo kuta na sakafu zake ni za vumbi kutakuwa na shida sana kwa wanafunzi kujibu mtihani huo kwani usafi wa hali ya juu unahitajika katika mfumo huo”anasema.

Mbali na hilo anasema kuwa baadhi ya shule nyingine wanafanya mitihani miwili au mitatu kwa kipindi chote ambacho wako katika maandalizi ya kufanya mtihani ya Taifa,ukiacha mtihani wa wilaya na mkoa huo wa Taifa.

Anaongezea kuwa mitihani mingine yote inayofanywa ndani ya shule hizo yote inaandikwa ubao hivyo mwanafunzi ajengewi mazingira mapema ya kuweza kujibu mtihani huo kwa mfumo huu mpya wa OMR.

“Najua mambo ya shule za vijijini kwani mimi mwenyewe nimesoma huko kijijini ambako shule moja ina walimu wawili au watatu na huu mfumo ni changamoto kubwa sana kwa wanafunzi wa huko vijijini,”anasema.

Anaongezea kuwa mbali na hayo  changamoto nyingine inayoikumba mfumo huo ni kwa wanafunzi kupata na wasiwasi wakati wa mtihani wa taifa na kusababisha kutoka jasho katika viganja vya mikono.

Anaongezea kuwa kitendo cha kutoka jasho mikononi kunahatari ya kulowesha karatasi hiyo na kusababisha kushindwa kuweza kusahihishwa kwa njia ya komputa na matokeo yake kusababisha mwanafunzi kufeli mtihani.

Wanafunzi kote nchini wameanza kufanya mtihani kwa kutumia mfumo mpya wa OMR huku baadhi yao wakiwa na uoga kwa sababu huu ni mfumo mpya, lakini je serikali imejipangaje kuzikabili changamoto ambazo zinaonekana kuukabili mfumo huo.

Mfumo unatija wa kuondoa tatizo la udanganyifu katika swala zima la mtihani je walimu wamejipanga kukabiliana nao au ndio itakuwa wanatafuta mbinu mpya ya udanganyifu wa mtihani.

Mtahiniwa wa darasa la saba katika shule ya Mchangani iliyopo Mwananyamala Dar es Salaam Scola Mbawala anasema kuwa mfumo huo kwao umekuwa unachangamoto kubwa kutokana na mazoezi waliyoyafanya ni ya muda mfupi.

Anasema kuwa muda ambao wamejifunza jinsi ya kujibu maswali kwa njia hiyo mpya haujatosha kwani wamejifunza kwa muda mchache sana tofauti na mazoea waliyoyazoea ya kujibu mtihani kwa njia ya kawaida.

Anasema kuwa njia hiyo inahitaji umakini zaidi kwani ukikosea na kama unatabia ya kufutafuta unakosa alama katika usahihishaji hivyo itasababisha wanafunzi wengi kufele kulingana na mazingira ambayo yapo katika shule zetu na uoga kwa baadhi ya wanafunzi.

“Mfumo huu ni raisi kufanya udanganyifu kwani ni rahisi mwenzio kuchungulia  majibu sehemu uliweka kivuli nay eye kufanya hivyo hiyo kwa mfumo huu bado udanganyifu utakuwa pale pale,” alisema

Serikali ina nia nzuri ya kumjengea uwezo mwanafunzi lakini iliweka angalizo la hizi changamoto ambazo zitaikumba mfumo huo ili uweze kuwa na tija kwa taifa letu.

No comments:

Post a Comment