24 September 2012

Kipaumbele cha watanzania ni nini?


NA Michael Sarungi

SIKU nilipo msikia Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa akishauri kuwa Elimu ndiyo inayofaa kuwa kipaumbele cha kwanza kwa Watanzania sikushangaa wala kusikitika.

Kwa mtazamo wa watu wasiotaka kujishugulisha na kufikiri wanaweza kumuona kiongozi huyu kama mtu ambaye ana tapatapa, lakini kwa uhalisia wa kimaendeleo bila ya watu wetu kuwa na elimu  tutakuwa tunajidanganya tu.

Mara baada ya Bw.Lowassa kutoa kauli hiyo kama kawaida kwa Watanzania wakajitokeza watu wenye mitizamo tofauti na kusema kuwa kiongozi huyo ameamua kupingana hadharani na mpango wa serikali.

Kwa upande wangu nakubaliana nao si kwa kuwa wamesema yaliyo ya kweli la hasha ila kwa sababu Katiba yetu ya Jamhuri inatoa uhuru wa kila mtu kutoa mawazo yake na kusikilizwa.

Tatizo kubwa ambalo linatukabili Watanzania kuanzia wa kawaida mpaka kwa viongozi wetu ni kutokukubali kujifunza toka kwa wenzetu ambao wamefaulu katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.

Takwimu nyingi toka katika nchi zilizoendelea zinaonyesha kuwa moja kati ya silaha kubwa iliyotumika kupambana na umasikini, maradhi na ujinga ni elimu na kwa upande mwingine nchi hizo zilihakikisha zinatilia mkazo katika kuwekeza rasilimali fedha na utaalamu katika sekta husika.

Hii wala haihitaji miujiza toka kwa wachungaji wetu ila ni kuwa na nia ya dhati na mitizamo ya kimaendeleo inayolenga kuwakwamua Watanzania toka kwenye umasikini.

Ukiangalia mifano mingi ya nchi nyingi zilizo endelea uatagundua kuwa hazikuhitaji miujiza zaidi ya kuwekeza kwa nguvu zote katika sekta ya elimu na kuhakikisha elimu hiyo inapatikana kwa wote bila ya kuruhusu matabaka.

Na ndiyo mwaana hata Mwalimu nyerere wakati wa utawala wake alitilia mkazo katika elimu kwa kuja na misemo mbalimbali kama elimu ni uti wa mgongo, elimu ni bahari, elimu ni ralimali na nyingine nyingi lengo likiwa ni kuhamasisha na kutilia mkazo katika elimu.

Serikali ya wakati huo ilijiwekea mipango mikakati ya kisera na kiitikadi, siasa ya ujamaa na kujitegemea ufahamu juu ya ukombozi wan chi zilizokuwa kusini mwa bara la kiafrika.

Mkazo wa kwanza kwa serikali hiyo ya awamu ya kwanza ulilenga ingalau watu wajue kwanza kusoma na kuandika hapa tunaona kuwa ilianzishwa mpango wa elimu ya watu wazima(ngubaru).

Lengo kuu ya yote haya ililenga watu wajue kuwa bila ya elimu ilikuwa ni vigumu sana wote kwa pamoja kuanza safari ya kusaka maendeleo kwa hiyo serikali hiyo iliamini katika ile dhana ya Lowassa kuwa Elimu kwanza na si Kilimo kwanza.

Maelezo hayo ya Bw.Lowassa aliyo yatoa hivi karibuni yanaakisi kwa kiwango kukubwa matokea chanya yaliyoisaidia nchi yetu kupata maendeleo ya haraka kuanzia miaka ile ya uhuru.

Kama walivyo sema wahenga wetu kuwa Taifa lisilo kuwa na elimu ni sawa na mfu hii yote ilikuwa ni katika kuchagiza umuhimu wa elimu, swali la kujiuliza hapa ni kwanini watu hawa walikuwa wakiifananisha elimu na vitu vyenye mashiko kama, ufunguo, hazina, raslimali na vingine vingi?

Hii ni kwa sababu pamoja na huo ukaliwao lakini bado walijua kuwa bila ya watu/ mtu kuwa na elimu hakuna chochote anachoweza kukifanya kinacho weza kumtoa au kumkwamua toka katika umasikini.

Waliamini kuwa kitendo cha kumpatia mtu elimu unakuwa unamuwezesha kimanisha na kumrahisishia kazi, humfanya aweze kujitegemea kiurahisi kwa kuweza kujifunza kiurahisi na kiufasaha.

Ukosefu huu wa elimu kwa Watanzania kuanzia kwa wakulima, wafugaji, warina asali, wavuvi na wengine wengi kwa kiwango kikubwa umechangia watu hawa kuzidi kuwa masikini kwa miaka nenda rudi japo tuna miaka hamsini tangu tupate uhuru.

Tanzania ya leo bado ni nchi iliyo jaa raslimali za kila aina lakini wananchi wake bado ni masikini wa kutupwa ambao hawajui kesho yao itakuwaje na wala hawana mategemeo yoyote.

Bado wakulima wetu baada ya miaka hamsini ya uhuru wameshindwa kubadilika hawajui hata kuchagua mbegu zinazofaa kwa maana nyingine ni kuwa bado hawajawa na elimu juu ya kilimo cha kisasa kinacho weza kuwabadilisha toka kilimo cha jembe la mkono na kutumia teknolojia ya kileo.

Hata upande wa sekta nyingine nako hali bado ni mbaya hebu angalia baada ya miaka hamsini ya uhuru bado wavuvi wetu hawana hata elimu ya kuelewa kuwa uvuvi haramu una madhara makubwa kwao na kwataifa zima hii yote ni ukosefu wa elimu husika.

Takwimu zinaonyesha kuwa kuna nchi nyingi ambazo zimepiga hatua ya kimaendeleo japo kuwa hazina raslimali nzuri kama ya ardhi, madini,bahari, mazima na misitu lakini kwa kuwekeza kwenye elimu wamepiga hatua za ajabu.

Ni upuuzi na uchafuzi wa raslimali ya Taifa kukimbilia kuwapa wananchi matrekta na pembejeo nyingine kabla ya kuwapa elimu ya jinsi ya kukiendesha kilimo hicho cha kisasa ni kazi bure.

Iwapo kweli serikali inania ya dhati kuleta mapinduzi ya kilimo ni bora kwanza tukaanza kuwekeza katika elimu kwa wakulima juu ya kile wanachotaka kufanya kuliko kuweka siasa katika mambo yetu.

Katika hili siyo kuwa mimi ni mpinzani wa maendeleo ya kilimo hapa nchini la hasha mimi ni muumini wa ukweli kuliko kuwa mnafiki usio kuwa na tija kwa wananchi.

Sasa Taifa linahitaji kuirejea visheni mpya itakayo tuwezesha kwa kila mmoja wetu kuanzia gazi ya kaya kwani huko ndiko mahali pa kufikiria jambo la kufanya  kama familia.

Tuanze kujipanga kuanzia kwenye kaya zetu kwa kibua njia, mikakati na mbinu za kutuwezesha kuwa mfano mzuri kwa wengine na kuwa kama mfano wa kuigwa kama tulivyo kuwa miaka ya nyuma.

Tuache tabia za kufikirika ya kuona kuwa siasa ndiyo mtaji pekee wa kimaendeleo na mbaya zaidi kwa viongozi wengi kujikita katika siasa na kusahau majukumu yao ya kila siku.

Wakumbuke kama nilivyo sema huko juu kuwa mataifa mengi yaliyoendelea yanatumia mda mwingi sana kuangalia jinsi wanavyo weza kuleta mabadiliko katika nyanja kama elimu kwa lengo la kuwanyanyua wananchi wake.

Ni kweli kilimo ndiyo sekta inayoongoza kwa kutoa ajira kwa watu walio wengi lakini ni ukweli usio pingika kuwa ukosefu wa elimu kwa wananchi juu ya kilimo kumechangia kwao kushindwa kupiga hatua.

Sisi kama raia tuendelee kukemea na kupambana na uovu rushwa na uonevu katika jamii yote inayo tuzunguka kwa upande wa serikali wahakikishe kuwa wanatekeleza majukumu yao na kuzifanyia kazi changa moto zinazo ibuliwa bila ya kuangalia aliye ziibua ni nani.

Wawe tayari kukosolewa kwa yale wanayo yafanya kwani kuwa kwao madarakani sio kuwa wamekamilika kwa kila jambo na mwisho wa siku wakae wakijua kuwa Taifa lisilo toa elimu kwa watu wake ni sawa na mfu.

Waanze kuwaeleza wananchi kuwa ili kufanikiwa katika kitu chochote unachotarajia kukifanya bila ya kuwa na elimu ya jambo lenyewe ni sawa na kazi bure na wajue kuwa Elimu kwanza na si Kilimo kwanza.



No comments:

Post a Comment