25 September 2012

Mbunge awaomba walimu wasifanye mgomo mwingine



Na David John

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Dar es Salaam kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bi. Phiripa Mturano, amewaomba walimu kutochukua uamuzi wa kugoma tena kwani waathirika wakubwa ni watoto wa maskini.


Bi. Mturano aliyasema hayo Dar es Salaam juzi katika mahafali ya tano ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Magnus, iliyopo Pugu, Maniuspaa ya Ilala.

“Nawaomba walimu msirudie kufanya mgomo kama mliofanya awali na kufikisha ujumbe wenu, jambo la msingi muwe na uvumilivu wakati madai yenu yakifanyiwa kazi,” alisema.

Aliongeza kuwa, uamuzi wa kugoma kufundisha utalifanya Taifa likose watalaamu ambao watachochea ukuaji wa uchumi wa nchi sambamba na kuwataka wahitimu kuwa na nidhamu.

“Kufeli mtihani kusiwafanye mkate tamaa ya maisha, kinachotakiwa ni kutuliza akili na kutafakali namna ya kuendelea na masomo au kujiendeleza kwa ujuzi mwingine,” alisema.

Mkuu wa shule hiyo, Bw. Charles Kayagwa, alisema jumla ya wanafunzi 70 wanatarajia kufanya mtihani huo Oktoba mwaka huu.

“Changamoto tulizonazo hapa shuleni ni pamoja na uchache wa vifaa vya kufundishia, kompyuta, mabweni ya wanafunzi wa kike na maabara waliyonayo kutojitosheleza hivyo naomba wananchi mjitokeze kutuchangia ili kuinua kiwango cha elimu,” alisema.

No comments:

Post a Comment