25 September 2012

TFF yazipongeza KRFA, MARFA


Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limevipongeza Vyama vya Mpira wa Miguu Mikoa ya Kilimanjaro (KRFA) na Manyara (MARFA) kwa kupata viongozi wapya katika chaguzi zilizofanyika mwishoni mwa wiki katika mikoa hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza vyama hivyo, unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa KRFA na ule wa MARFA, walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo katika mikoa hiyo.

Alisema wanaahidi kuendeleza ushirikiano kwa Kamati za Utendaji za MARFA na KRFA zinazoongozwa na Elley Mbise na Goodluck Moshi, kwani viongozi hao wapya wana changamoto nyingi kubwa, ikiwa ni kuhakikisha wanaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba zao na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yao.

"Pia tunatoa pongezi kwa Kamati za Uchaguzi za IRFA na MARFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF," alisema Wambura.

Viongozi waliochaguliwa kuongoza MARFA ni Elley Mbise (Mwenyekiti), Wilson Ihucha (Makamu Mwenyekiti), Apollinary Kayungi (Katibu), Peter Abong'o (Mhazini), Khalid Mwinyi (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Phortinatus Kalewa (Mwakilishi wa Klabu TFF) na Peter Yaghambe (Mjumbe).

Kwa upande wake KRFA waliochanguliwa ni Goodluck Moshi (Mwenyekiti), Mohamed Mussa (Katibu), Kenneth Mwenda (Mwakilishi wa Klabu TFF), Kusiaga Kiyata (Mhazini) na Denis Msemo (Mjumbe).

Aliongeza nafasi zilizowazi baada ya kukosa wagombea wenye sifa kwenye vyama hivyo zitajazwa baadaye.


No comments:

Post a Comment