17 September 2012

Malindi yazidi kufanywa kichwa cha mwendawazimu


Na Mwajuma Juma, Zanzibar

TIMU ya Soka ya Malindi, imeendelea kuchapwa katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu ya Zanzibar baada ya kufungwa na KMKM mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan juzi.

Hiyo ni mechi ya pili mfululizo kwa Malindi kupoteza tangu ligi hiyo inayodhaminiwa na kinywaji cha Grand Malt kuanza Septemba 8, mwaka huu.

Katika mchezo huo KMKM ambao walifungwa na Mafunzo katika mchezo wao wa kwanza bao 1-0, walilazimika kutumia nguvu za ziada ili kuweza kufuta machungu hayo na kufanikiwa kuondoka na pointi tatu muhimu uwanjani hapo.

KMKM walijipatia mabao yake kupitia kwa wachezaji Mudriki Muhibu katika dakika ya 47 na Maulid Ibrahim Kapenta aliyefunga katika dakika ya 90 za mchezo huo.

Kwa upande wa Malindi, bao lao la kufutia machozi lilifungwa na
Issa Hamad dakika moja tu baada ya kipyenga cha mechi hiyo kupulizwa kipindi cha kwanza.

Mbali na mchezo huo, pia huko Kisiwani Pemba, mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Super Falcon nayo ilifungwa na Duma mabao 2-1 ambapo mabao ya Duma yalifungwa na Salum Abdallah huku la Super Falcon likifungwa na Mohammed Salum.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo kwa mchezo mmoja
utakaowakutanisha Mtende Rangers na Mundu ambao utachezwa kwenye
uwanja wa Amaan.

No comments:

Post a Comment