28 September 2012

Makachero kumchunguza Mbunge CCM



Na Peter Mwenda

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi kutuma makachero wake kufanya uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili Mbunge wa Viti Maalumu, mkoani Pwani, Bi. Zainab Vullu na wenzake ili kujua kama wanahusika na vitendo vya rushwa.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Taifa, Bw. Nape Nnauye, alisema hajui ni lini wataanza kazi hiyo lakini ikibainika walihusika, chama hakitasita kumvua uanachama mtu aliyepokea au kutoa rushwa.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), jana ilimuita Bi. Vullu na kumuachia.

Inadaiwa kuwa, katika kikao cha Baraza Kuu la UWT Wilaya ya Kisarawe, kilichohudhuriwa na wajumbe 49 kutoka kata 15, maofisa wa TAKUKURU walivamia kikao hicho na kukamata sh. 550,000 ambazo zinadaiwa zilikua zitolewe kwa wajumbe.

Mbali ya fedha hizo, maofisa hao waliondoka na nyaraka mbalimbali zilizokuwepo mezani ambapo Kamanda wa TAKUKURU mkoani Pwani, Bi. Joyce Shirima, alikiri kutokea tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa baada ya uchaguzi kukamilika.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Bi. Vullu alikana kukamatwa na rushwa kwani yeye alikuwa mjumbe mwalikwa kama wengine hivyo alistahili kupata posho na chakula na jana alithibitisha kuhojiwa na TAKUKURU kisha kuachiwa.

No comments:

Post a Comment