10 September 2012

Majambazi waua, wajeruhi wanne


Na Daud Magesa, Mwanza

MTU mmoja ameuawa na wengine wanne kujeruhiwa kwa kupigwa mapanga na kundi la watu wanaodhaniwa kuwa majambazi baada ya kuvamia maduka matano yaliyopo eneo la Bushitu, Kata ya Igoma, Wilaya ya Nyamagana, nje kidogo ya Jiji la Mwanza.

Tukio hilo limetokea usiku wa kumakia jana ambapo zaidi ya sh. milioni 1.5 ziliporwa na simu 45 za mkononi zenye thamani ya sh. 400,000 kutokana kwa wafanyabiashara wa maduka hayo.

Inaelezwa kuwa, majambazi hao zaidi ya 10 wakiwa na bunduki moja na silaha za jadi pia waliwajeruhi baadhi ya watu waliokwenda eneo hilo kutoa msaada kwa wafanyabiashara.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Barlow, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, majambazi hao walikimbia baada ya kusikia mngurumo wa gari la polisi.

Alisema wananchi walichelewa kutoa taarifa na kusababisha askari wachelewe kufika ambapo majambazi walipobaini polisi walikuwa karibu kufika eneo hilo walikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Mjumbe wa nyumba 10, Mtaa wa Bushiru, Bw. Mihaga Mang’ombe, alisema tukio hilo lilitokea saa saba usiku ambapo majambazi hao walivamia na kupora maduka matano.

Alisema majambazii hao waliwajeruhi watu watano sehemu mbalimbali za mwili kwa mapanga walipokwenda kutoa msaada ambapo katika tukio hilo, mtu mmoja ambaye hajafahamika jina, mwenyeji wa Kijiji cha Butuguri, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara, alijeruhiwa na alifariki dunia akiwa Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC), alikopelekwa kupatiwa matibabu.

Majeruhi waliolazwa katika hospitali hiyo ni Bw. Peter Ndalahwa, Bw. Adam Kizaba na wengine ambao wametambuliwa kwa jina moja moja, Amran na Amidam, wote wakazi wa Mtaa wa Bushiru.

No comments:

Post a Comment