18 September 2012

Lugalo vishale watwaa ubingwa wa Safari Darts



Na Mwali Ibrahim

KLABU ya Lugalo ya mchezo wa Vishale imetwaa ubingwa wa mashindano hayo yaliyojulikana kwa  jina la  'Safari Darts Dar Clubs Championship 2012' kwa kupata pointi 18 katika mashindano yaliyofanyika juzi.

Lugalo walitwaa ubingwa huo na kuzawadiwa kikombe na fedha taslimu sh.300,00 na Meneja Mauzo wa bia ya Safari wa Kinondoni na Ilala, Victor Kavishe ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mashindano hayo.

Mshindi wa pili katika mashindano hayo ni klabu ya Upanga ambayo ilipata pointi 16 na wa tatu ni Polisi Balax ambao walipata pointi 13.

Mashindano hayo yaliendeshwa kwa mfumo wa ligi mpaka washindi kupatikana, na klabu zilizoshiriki ni  Lugalo, Upanga, Polisi Balax, Freinds, Magereza, Mbezi Beach,Kashudu,Kawe na Kimanga.

Lugalo inashika nafasi hiyo huku ikiwa tayari ilishatwaa nafasi ya pili katika mashindano ya Afrika Mashariki yaliyomalizika hivi karibuni.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kukabidhi zawadi hizo Kavishe alisema Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) , kupitia kinywaji chake cha ya Safari Lager iko bega kwa bega na mchezo wa Darts, kuhakikisha inasaidia kwa kila linalowezekana kuuendeleza na kuukuza mchezo huo hapa nchini.

Pia aliwapongeza washiriki wote kwa utulivu mpaka washindi kupatika kwa amani, na kuwataka kuzidi kujiweka sawa kwa ajili ya kuendeleza mchezo huo.

Naye katibu wa Darts Mkoa wa Dar es Salaam, Lambarth Rwihula aliwashukuru Safari Lager kwa ufadhili wao na kuyaomba makampuni mengine yaige mfano huo.

No comments:

Post a Comment