24 September 2012

Kikongwe anyang'anywa ardhi



Na Bryceson Mathias,Dodoma

KIKONGWE wa Miaka 80 Bibi.Mdala Lusinde wa Kata ya Mbabala,mkoani Dodoma ameangua kilio kulaani kitendo cha Baraza la kata kumnyang'anya ardhi yake anayoitegemea impatie chakula.

Huku akilia Bibi.Mdala alimweleza Mwandishi wa Gazeti hili jana kuwa, hivi sasa baadhi ya uongozi wa vijana, unapuuza kila kitu kinachofanywa na wazee na kutojali ushauri wala mawazo yao,hivyo kila kinachofanywa nao kinaonekana hakina maana na
walicho nacho wananyang’anywa kwa visingizio.

Bibi. Mdala huku akiendelea kuomboleza kwa kilio alilaani kitendo cha Baraza la Kata kutumia hila ya nyadhifa zao kumnyang'ang’anya ardhi yake
iliyokuwa ikimpatia chakula aweze kujikimu kimaisha.

Alisema kuwa ardhi hiyo amegawaiwa Bw.
Mikae Mikuya ambaye inadaiwa aliuziwa na Marehemu mume wake Bw. Yona Ndallu,ambapo alidai kuwa hati za mauziano ni batili na bandia.

“Mume wangu miaka yote hadi anatwaliwa na Mungu na kuniacha, hakujua kusoma na kuandika na hakuwahi kushika Kalamu na kuandika, nashangaa kusikia uongozi wa Baraza la Kata ulimpatia Ardhi hiyo Kijana Mikuya zikiwa zimesainiwa, je alizisaini nani? Mume wangu hakujua kusoma, na nilipaswa kujua kinachojiri," alihoji.

Katibu wa Baraza la Kata Bw. Shamte Ibrahimu alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo kwamba, kwa nini walitoa maamuzi wakitumia hati bandia, alikiri makubaliano hayo yalikuwa ya miaka minne iliyopita, ambapo alidai mtu aliweza kuwekewa sahihi na mtu
mwingine katika uuzaji wa ardhi, jambo ambalo lilipingwa na Bibi.Mdala, huku Bw.Ibrahimu akionekana anapwaya kwa uelewa wa sheria.

“Mdala
Lusinde ni Mkorofi, Mume wake alishauza Shamba hilo miaka minne iliyopita kwa
kuwekewa sahihi na mtu mwingine kwenye hati ya mauzo,…lakini mimi ni mgeni si
msemaji …..”Katibu wa Baraza Bw. Ibrahimu alibabaika alipobanwa na mwandishi.

Mwandishi alimtafuta aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Vilindoni lilipouzwa shamba
Bw. William Mgale yeye alipinga hatua iliyofanywa na Baraza la Kata kuwa, Shamba hilo ni haki ya Kikongwe huyo, na akathibitisha kwamba, katika moja ya kesi zilizowakilishwa kwenye uongozi wake, ilibainika hati ya mauzo iliyotolewa na Bi.
Anatolia Daudi ni Bandia, na sahihi iliyopo si ya marehemu Bw. Ndallu, kwa sababu hakujua kuandika na mkewe hakuhusishwa.

Katika kutaka kujua uhakika wa suala hilo Mwandishi wa habari hizi pia alimtafuta Diwani wa Kata ya Mbabala Bw. Amosi Makasi ambaye alidai kuwa
anamfahamu vizuri Kikongwe Mdala kuwa si mtu mkorofi kama inavyodaiwa.

Alisema kuwa hakuna taarifa iliyofikishwa kwake ya kunyang'anywa shamba mezani kwake, hivyo kuahidi kufuiatilia kuhakikisha uzee dawa wa akina Mdala na wengine, wanaheshimiwa katika uzee wao badala ya kuwapuuza na kuwadhulumu.



No comments:

Post a Comment