24 September 2012

Makete afunguka kuhusu tuhuma


Na Mwandishi Wetu

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake, Wilaya ya Kinondoni, Bibi Anna Luvanda ‘Mama Makete’ amesema wanaomzushia kwamba yeye ndiye chanzo cha migogoro ya ardhi wilayani Kinondono ni za kupikwa na zimeibuliwa kwa malengo ya kisiasa.

Mama Makete ambaye amekuwa akiandamwa na watu wanaotaka kubomoa nyumba na kupora kiwanja chake, hivi karibuni alizushiwa tuhuma nzito kwamba anafuga majambazi kwa ajili ya kuvamia mashamba ya watu na anawapa fedha wanawake na watoto na kuwapakia kwenye magari yake na kuwatelekeza karibu na Ikulu ya Rais Kikwete.

Mama Makete alizushiwa amekuwa akifadhili wananchi waliovunjiwa maeneo hayo kwa kuwapatia hifadhi katika eneo la machimbo ya kokoto ambako wameweka kambi.

Pia anadaiwa kumiliki machimbo ya kokoto na ndiye mfadhili mkuu wa vijana wanaoendesha vitendo vya kihuni katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mama Makete ambaye ni mjane alisema madai yaliyoelekezwa kwake si ya kweli bali yameibuliwa na  wajanja wanaopanga mikakati ya kutaka kubomoa nyumba yake na malengo ya kisiasa.

“Wamenizushia mambo mengi. Wengine wanasema ni jambazi, hivi mwanangu, kweli mimi nafanana na majambazi? Hapa nyumbani kwangu naambiwa nafuga majambazi, umeingia, umeona, kuna dalili za kuwepo majambazi. Mimi naonewa bure labda sijui kwa vile wameniona mjane?” alihoji kwa masikitiko Mama Makete.

Alisema kundi linalotaka kubomoa nyumba yake na kumpora eneo hilo kisiasa, limekuwa likitumia fedha kwenye vyombo vya habari kupotosha ukweli huku wakifungua kesi kiunjanja bila kumpa samansi, ili shauri lisikilizwe upande mmoja.

Akizungumzia ujanja unaotumika katika kufungua shauri hili, Mama Makete alisema mwaka 2008, walalamikaji walifunguliwa kesi ya madai katika Mahakama ya Nyumba kata ya Kunduchi wakidai eneo hilio.

Alisema kesi hiyo ilifunguliwa na Elizabeth Chacha na Ranger Daniel dhidi ya Castro Mwajala na Ally Mgulu na eneo linalodaiwa ni la ekari nne.

Katika uamuzi wake Novemba 11, mwaka huo Mwenyekiti wa Baraza hilo la Ardhi la Kata ya Kunduchi, Bernadeta Kagoswe na wajumbe wake walisema hawakuona kisima wala mazao ya kudumu kama mashahidi wa walalamikaji walivyodai.

Kwa hali hiyo aliamuru shauri hilo lipelekwe kwa Mwenyekiti wa Ardhi na Nyumba Wilaya ya Kinondoni, kwani tayari kuna hati na thamani yake ni kubwa.

Kwa mujibu wa Mama Makete, Septemba 30 mwaka 2009, kesi hiyo ilikuja tena, lakini kwa mara nyingine walalamikaji na walalamikiwa wote hawakufika.

“Shauri lilikuja tena Desemba 4, mwaka 2009 pande zote hazikufika na lilikuja tena Januari 22 mwaka 2010, chini ya Mwenyekiti wa Baraza R.L David, wahusika pia hawakutokea,”.

“Sisi tulikuja kupata taarifa ya shauri hili badaye. Hata hivyo lilifutwa kwa sababu wahusika wa pande zote hatukuwa tunafika mahakamani,” alisema Mama Makete.

Kwa mujibu wa Mama Makete, miaka miwili baadaye, shauri hili liliibukia Mahakama Kuu na kama ilivyokuwa katika Baraza la Ardhi la Wilaya, walalamikaji hawakupata samansi na walalamikaji pia hawakuwa wanahudhuria siku za kutaja kesi, hivyo mahakama iliamua kuliondoa shauri hilo.

“Tunavyozungumza na wewe, shauri hili limerudishwa tena Baraza la Ardhi la Kinondoni na Oktoba 10 huenda amri ya kubomolewa nyumba zetu, ikatolewa.”

Mama Makete amemuomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kuingilia kati suala hilo ili kukata mzizi wa fitna.

No comments:

Post a Comment