28 September 2012

JK: Mkulima mdogo athaminiwe


Na Queen Lema, Arusha

RAIS Jakaya Kikwete amesema Afrika haiwezi kupata maendeleo makubwa bila kumshirikisha mkulima mdogo ambaye anakabiliwa na changamoto nyingi ambazo peke yake hawezi kupambana nazo.

Alisema mkulima mdogo katika nchi za Afrika ameendelea kutumia zana za jadi kama jembe la mkono ambalo haliwezi kumsaidia apige hatua ya maendeleo kutokana na changamoto alizonazo.

Rais Kikwete aliyasema hayo mjini Arusha juzi alipokutana na
alipokutana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani katika Afrika (AGRA), Bw. Kofi Annan, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN).

Bw. Annan yupo nchini akishiriki mkutano wa pili wa AGRA ambao umefunguliwa na Rais Kikwete ambao agenda kuu ni kujaribu kuleta mageuzi ya kilimo Afrika. Mkutano wa kwanza ulifanyika nchini Ghana miaka miwili iliyopita.

Alisema huwezi kuzungumzia maendeleo ya aina yoyote katika Afrika bila kumshirikisha mkulima mdogo.

“Uchumi wetu unakua kwa kasi ya kuridhisha hasa katika sekta za mawasiliano, miundombinu, madini na utalii lakini mafanikio bado hayajaanza kuonekana wazi kwa wananchi kwa sababu kilimo ambacho ndio kinaajiri Watanzania wengi, kasi ya ukuaji wake ni ndogo na kumvuta kila mmoja kurudi chini,” alisema.

Kwa upande wake, Bw. Annan alimsifu Rais Kikwete kwa uongozi shupavu katika eneo la kilimo kutokana na programu mbali mbali ambazo Serikali yake imezianzisha.

“Nakupongeza sana Mheshimiwa Rais Kikwete kwa uongozi wako makini kwani umekuwa mfano wa kuigwa katika Bara letu hasa katika eneo hili la kilimo,” alisema Bw. Annan.

Akifungua mkutano huo, Rais Kikwete alizitaka nchi za Afrika kuboresha vituo mbalimbali vya utafiti wa kilimo ili kukabiliana na changamoto zilizopo.

Alisema sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto nyingi katika nchi mbalimbali ambazo zinahitaji utatuzi wa haraka kupitia vituo vya utafiti na kutoa elimu ya kilimo cha kisasa kwa wakulima.

Naye Bw. Annan alisema ni vyema wadau wa sekta umma na binafsi waone umuhimu wa kuwekeza katika Kilimo na kama watafanikiwa kufanya hivyo wataimarisha sekta hiyo na kukuza uchumi.

“Serikiali za Afrika nazo ziwekeze katika kilimo, kuwasaidia wakulima wadogo na wakubwa hasa kwa kuwapa mahitaji muhimu ambayo mara nyingine wanayokosa hali inayochangia washindwe kufikia malengo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment