28 September 2012
Wizara: Watakaovuruga maombi ya uwekezaji vitalu kuchukuliwa hatua
Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Maliasili na Utalii, itawachukulia hatua watu wote ambao watakiuka sheria, kanuni na taratibu za utekelezaji mchakato wa kuwapata wawekezaji katika vitalu vilivyopo kwenye maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori (WMAs).
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Bw. Paul Sarakikya, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua warsha ya mafunzo kuhusu mchakato wa kufungua maombi ya uwekezaji kwenye vitalu vya WMAs.
Alisema mchakato huo ambao ni nyeti unaohitaji umakini mkubwa katika kuutekeleza, utahusisha watu wenye uwezo wa kifedha hivyo unaweza kusababisha uwepo wa mazingira ya rushwa.
Aliongeza kuwa, kushindwa kuzingatia vigezo vitakavyokubalika katika mchakato huo, kutasababisha migogoro isiyo ya lazima hivyo kudhoofisha maendeleo ya jumuiya na kukatisha tamaa vijiji vilivyotenga maeneo ya kuanzisha WMAs.
“Napenda kusisitiza kuwa, kanuni za WMAs zinazitaka jumuiya kufanya uteuzi wa wawekezaji kwa kutumia vigezo vilivyotumiwa na Wizara kuwapata wawekezaji kwenye vitalu vyake.
“Vigezo hivyo viko kwenye Kanuni za Uwindaji wa Kitalii (2010), kifungu cha 10(2), hivyo washiriki watapata fursa ya kuvipitia na kuviwekea alama kwa kuzingatia mahitaji na hali halisi ya WMAs,” alisema Bw. Sarakikya.
Alisema Wizara hiyo itashirikiana na vyombo vya dola kufuatilia utekelezaji wa mchakato huo na haitasita kuwachukulia hatua wote walioshindwa kuweka mbele masilahi ya jumuiya zao na ya Taifa kwa Ujumla.
Bw. Sarakikya alisema kwa kutambua umuhimu wa mchakato huo, Wizara imetoa Ofisa kutoka Kitengo cha Matumizi Endelevu ya Wanyamapori ili kutoa mafunzo.
“Wizara inatarajia wajumbe wote watakubalina na kuhitimisha hatua za kimchakato zitakazotumika na hatimaye kuwa na mwongozo utakaotumika na kamati ambazo zitafungua maombi hayo,” alisema.
Warsha hiyo imelenga kuwawezesha wajumbe kupata uelewa wa pamoja wa nini cha kufanya baada ya jumuiya zilizo hizo kupokea maombi ya uwekezaji katika vitalu vya WMAs kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori namba tano ya mwaka 2009 na Kanuni za WMAs 2012.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment