28 September 2012

Nkya akabidhi kijiti kwa Msoka, Majira lapewa cheti cha shukrani


Na Darlin Said   

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari nchini (TAMWA), Bi. Ananilea Nkya, jana amekabidhi kijiti kwa Mkurugenzi mpya wa chama hicho Bi. Valerie Msonga, katika hafla iliyofanyika kwenye ofisi za chama hicho zilizopo Sinza.


Akizungumza kabla ya kukabidhi ofisi, Bi. Nkya alisema lengo la kuanzishwa chama hicho ni kutetea mabadiliko, haki za wanawake, watoto na Watanzania kwa ujumla.

Alisema upo umuhimu wa Watanzania kushikamana ili kutetea haki zao za msingi kwa mujibu wa shiria bila woga wowote ambapo hali hiyo itasaidia kuleta mabadiliko na kuchochea maendeleo.

“Naviomba vyombo vya habari viendelee kutoa habari zinazohusu maendeleo ya nchi, lazima wanawake tusimame kutetea haki zetu pamoja na zile za watoto wetu bila woga, tusipofanya hivyo hakuna anayeweza kufanikisha dhamira yetu ya mabadiliko,” alisema.

Kwa upande wake, Bi. Msoka, alimpongeza Bi. Nkya kwa kuiwezesha TAMWA ifahamike kitaifa na kimataifa pamona na kutekeleza majukumu ya chama hicho kwa mujibu wa katiba yao.

Alisema kazi iliyopo mbele yake kwa sasa ni utekelezaji mradi wa miaka miwili kujenga usawa wa kijinsia na kutokomeza vitendo vyote vya ukatili dhidi ya wanawake nchini.

“Mpango mkakati wetu ni kuangalia mchango wa TAMWA katika kushirikisha wanawake wanashiriki kutoa maoni yao kwenye mchakato wa kupata Katiba Mpya tunayoitaka.

“Utekelezaji wa majukumu yangu yatatokana na ushirikiano mkubwa ambao nitaupata kutoka kwenye vyombo vya habari, wanachama wenzangu wa TAMWA pamoja na wadau kutoka mashirika mengine ya ndani na nje yanayohusiana na sera za wanawake, watoto na haki za binadamu,” alisema Bi. Msoka.

Alisema kwa kutambua umuhimu huo, wanahitaji msaada wa mawazo kutoka kwa makundi ya watu mbalimbali ili kuboresha utendaji kazi wao kwa Watanzania.

Katika hafla hiyo, TAMWA ilitoa vyeti vya kutambua mchango wa vyombo vya habari nchini (likiwemo Majira), ambavyo ndivyo vimekiwezesha chama hicho kupata mafanikio makubwa waliyonayo.

Pia Bi. Nkya naye alipewa cheti ya kutambua mchango wake kwa kuiwezesha TAMWA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kujulikana kitaifa na kimataifa.

No comments:

Post a Comment