07 September 2012

Elimu itolewa kudhibiti uharibifu hifadhi za Taifa


Na Florah Temba

HIVI hii ni Kilimanjaro kweli, au nimekosea? Nilijikuta nikijiuliza maswali hayo mara baada ya kutinga katika  mkoa huo na kushuhudia uharibifu wa mazingira uliokuwa unaendelea.

Nikiwa nimepigwa na butwaa nikijiuliza maswali hayo huku nikichoshwa na kazi ya kufuta jasho, ghafla niliona watu kadhaa wakinishangaa bila kuzungumza.

Hali hiyo iliniongezea maswali kichwani mwangu, kwa nini watu hawa wananishangaa, nini nimekosea? Nilihamaki huku nikiendelea kuteseka na kazi ya kufuta jasho mwilini hasa kwenye uso wangu ambao ulionekana kama umemwagiwa maji.

Ndipo nilipojitazama mara mbili na kujigundua kuwa nilikuwa tofauti, hali ambayo ilinifanya nianze kupanguza nguo moja kwani zilinichosha na kunifanya nitote mwili mzima.

Wakati nikiendelea kuwaza, ghafla  nilizinduka kwenye mawazo na kuanza kujiuliza maswali mengine, ni nini kilichotokea katika mkoa huu, mbona watu hawavai makoti kujikinga na baridi? au ndio kusema wamehamia jangwa la sahara.

Wazo likanijia ni kutokana na mazingira kuharibiwa  kwa  kukatwa miti hovyo, kilimo kisichozingatia sheria na taratibu pamoja na uchomaji moto kwa ajili ya urinaji asali.

Maswali  na majibu hayo  yalinifanya ni ahirishe safari yangu niliyokuwa nayo na kuanzisha safari nyingine ya kwenda kwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama  ili kujua kulikoni.

Anasema, hali ya hewa katika mkoa wa Kilimanjaro imebadilika kutokana na sababu mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangiwa na shughuli za binadamu.

Anasema moja ya sababu zinazochangia mabadiliko ya hali ya hewa Mkoani Kilimanjaro, ni uharibifu wa mazingira ambao unatokana na ukataji miti hovyo, ulishaji wa mifugo kiholela kusikozingatia sheria na taratibu za mazingira, kilimo kisichozingatia sheria hadi kwenye kingo za mito na vyanzo vya maji pamoja na upasuaji mbao katika misitu ya hifadhi kinyume cha sheria.

Bw. Gama anasema katika kipindi cha mwaka huu, uharibifu wa mazingira umeleta athari kubwa katika mkoa huo ikiwa ni pamoja na kuwepo na mabadiliko makubwa  ya hali ya hewa, barafu ya mlima Kilimanjaro kupungua kwa zaidi ya asilimia 70 na joto kuongezeka hadi kufikia nyuzi joto 40 hali ambayo haijawahi kutokea.

Anasema athari nyingine ni mvua kutonyesha kwa wakati kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo, hali iliyosababisha mkoa huo kugubikwa na tatizo la njaa, mito na vyanzo vya maji kukauka  na kusababisha baadhi ya maeneo ikiwemo mji wa moshi kuingia katika historia ya kuwa na mgao wa maji.

Anasema kutokana na tatizo hilo mkoa huo umepiga marufuku ukataji miti na kuzuia utoaji wa vibali kwa ajili ya kukata miti kwa matumizi yote ikiwemo upasuaji mbao.

Anasema katika kukabiliana na tatizo hilo mkoa huo umeanza kuchukua hatua za makusudi ikiwa ni pamoja na kupanda miti ambapo katika kipindi cha mwaka huu umejiwekea malengo ya kupanda miti Mil.8.2 katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye kingo za mito na kwenye vyanzo vya maji linalengo likiwa ni  kurudisha uoto wa asili ndani ya mlima na kuufanya mkoa huo kurudi kwenye hali yake ya ubaridi kama zamani.

Anaeleza kuwa jitihada nyingine wanazochukua ni pamoja na  halmashauri zote za wilaya mkoani humo kusimamia sheria za mazingira na kuhakikisha watendaji na wananchi wanafuata sheria hizo kikamilifu.

Jitihada nyingine ni kurudisha usimamizi wa msitu wa nusu maili kwa hifadhi ya mlima Kilimanjaro Kinapa, ili kuhakikisha miti inatunzwa na uoto wa asili unarudi kama zamani, pamoja na shule zote za msingi, sekondari, ofisi zote za serikali na taasisi zote kuanzisha vitalu vya miti.

“Ni kweli kwamba kuna uharibifu mkubwa wa mazingira katika mkoa huu hasa katika mlima Kilimanjaro, ambao kwa kiasi kikubwa unachangiwa na shughuli za binadamu, na kutokana na hili sasa kinapa iliyopewa dhamana ya kulinda mlima huu, inapaswa kuchukua hatua za makusudi kudhibiti uharibifu huo ili kuweza kuunusuru mlima huu ambao kwa sasa uko hatarini,” anasema Bw.Gama.

Bw.Gama anasema ni vema pia hifadhi hiyo ikaweka  mpango mkakati wa kudhibiti uhribifu katika mlima Kilimanjaro, ikiwemo matukio ya ujangili na uchomaji moto pamoja na kudhibiti mifugo wanaoingia msituni.

Mhifadhi mkuu wa hifadhi ya Kilimanjaro (KINAPA) Bw. Erastus Lufungulo anaanza kwa kusema, hifadhi hiyo ni moja ya hifadhi 15 zilizopo chini ya shirika la hifadhi ya Taifa Tanzania (TANAPA) na ni moja ya vivutio vya utalii hapa nchini.

Bw. Lufungulo anasema hifadhi hiyo ipo kaskazini mashariki mwa Tanzania yapata Kilometa 330 kusini mwa mstari wa Ikweta na ilianzishwa kwa ajili ya kuhifadhi mlima Kilimanjaro, madhari yake, maliasili zake, mfumo wake wa kiikolojia na uwezo wake wa kuhifadhi na kupokea maji.

Anasema ni mlima wenye vilele vitatu ambavyo ni Shira  chenye urefu wa mita 3,992, Mawenzi chenye urefu wa mita 5,149 na Kibo chenye urefu wa mita 5,895 kutoka usawa wa bahari na katika vilele hivyo vitatu vya mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika kilele cha Shira ni volcano iliyokufa wakati kilele cha mawenzi na kibo ni volcano zilizo lala na kwamba  ilifunguliwa rasmi kwa shughuli za utalii mwaka  1977 na mwaka 1989  ilitangazwa kuwa eneo la urithi  wa dunia (World Heritage Site).

Anasema pamoja na hifadhi hiyo kuwa moja ya vivutio vya utalii nchini Tanzania, kwa sasa inakabiliwa na tatizo kubwa la uharibifu wa mazingira yanayozunguka hifadhi hiyo, hali ambayo ni hatari  kwa usalama wa mlima Kilimanjaro ambao ni urithi wa dunia.

Anasema umaarufu wa hifadhi hiyo ni mlima mrefu kuliko yote barani afrika na ni moja ya milima mirefu iliyosimama kipekee duniani, pamoja na kuwepo kwa barafu nyingi ya kudumu katika kilele chake cha kibo  katika ukanda wa Ikweta na kanda tano tofauti za uoto wa asili tokea chini ya mlima hadi kileleni, na msitu mkubwa wa asili wenye baadhi ya mimea na wanyama ambao ndio unaharibiwa na majangili.

“Mlima huu  ni maarufu kama chanzo kikubwa  na muhimu sana cha maji kwa shughuli za kiuchumi na kijamii, na kivutio cha mlima huu ni maumbile yake ya kijiolojia (ukubwa, urefu na kilele chenye barafu), uoto wa asili, wanyama na hali ya hewa, lakini sasa wapo baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakivamia maeneo ya msitu huu na kukata miti ovyo au kuchoma moto hasa nyakati za usiku, na hii ni hatari sana kwa usalama wa mlima huu,” anasema Bw. Lufungulo.

Anabainisha kuwa zaidi ya vijiji 50 viko katika eneo la kuzunguka hifadhi ya mlima huo na kwa sasa wananchi wa vijiji hivyo wamepoteza utamaduni wa kulinda na kuhifadhi mazingira na badala yake nao wamejiingiza kwenye vitendo vya ukataji miti katika hifadhi kinyume cha sheria.

Bw. Lufungulo anasema pamoja na shughuli za uhifadhi mazingira ya mlima Kilimanjaro na doria ambazo zimekuwa zikifanywa katika maeneo mbalimbali ya mlima hasa katika msitu wa asili bado kumekuwepo na matukio ya ujangili ya uharibifu wa mazao ya misitu ambayo yamekuwa yakijitokeza katika hifadhi hiyo.

Anasema katika kipindi cha mwaka 2009  hadi juni 2012 matukio ya ujangili ya uharibifu yaliyojitokeza katika hifadhi ni pamoja na uwindaji haramu wa wanyama, uvunaji haramu wa miti kama ukataji fito, kuni, nguzo na upasuaji mbao pamoja na ulishaji haramu wa mifugo na uchomaji  moto ndani ya msitu.

Anasema tatizo sugu ambalo limekuwa likijitokeza ni upasuaji haramu wa mbao maeneo ya msitu  wa asili yanayopakana na vijiji vya Kibosho Sungu, Uru Njari, Uru shimbwe, Kieri, Nkweshoo, Kilema na Kishisha.

Anasema takwimu zinaonyesha kuwa majangili 420 wamekamatwa katika hifadhi ya KINAPA katika kipindi cha julai 2011 hadi Juni 2012  wakiwa wanajihusisha na uharibifu wa mazao ya misitu ikiwa ni pamoja na  ukataji wa miti ya asili.

Anasema pamoja na majangili hao pia zimekamatwa mbao 5,018, Chainsaw nane pamoja na bunduki tatu katika hifadhi jambo ambalo ni kinyume cha sheria za misitu.

Anasema ili kukabiliana na tatizo hilo wameanzisha ushirikiano na polisi mkoani Kilimanjaro ili kuongeza nguvu katika operesheni ya kuwakamata majangili hao ambao wamekuwa kikwazo kikubwa katika kulinda na kuhifadhi mlima Kilimanjaro.

“Hali ya ujangili katika maeneo ya hifadhi bado ipo na ujangili ambao umekuwa ukiendelea ni wa wanyama, mazao ya misitu na vipusa lakini tumejipanga kikamilifu kukabiliana na matukio hayo ili kulinda mlima wetu,” anasema.

Anasema pamoja na matukio hayo kuendelea, hifadhi hiyo kwa kushirikiana na polisi wamejipanga kupunguza tatizo hilo kama si kulimaliza kabisa kwa kuongeza nguvu katika operesheni na kuhakikisha kuwa kabla ya uhalifu kutokea watuhumiwa wanakamatwa kwani inakuwa vibaya kumkamata jangili wakati ameshafanya uhalifu.

Bw.Lufungulo anasema tatizo lingine ni  ulishaji mifugo ndani ya hifadhi ambalo limekuwa likisababisha madhara makubwa kwa hifadhi ikiwa ni pamoja na kuharibiwa kwa uoto wa asili.

Anasema mifugo 150 imekamatwa katika hifadhi hiyo katika kipindi cha Februari hadi Agosti mwaka huu jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa mazingira na rasilimali zilizopo katika msitu.

Anasema kunahitajika juhudi za makusudi za kunusuru mlima huo ambao barafu yake imeanza kupotea na kwamba juhudi hizo zinapaswa kufanywa kwa ushirikiano wa  serikali na wananchi wote wanaozunguka mlima huo.

“Barufu iliyopo katika kilele cha mlima Kilimanjaro ndiyo kivutio kikubwa cha utalii katika hifadhi hii, na endapo barafu hiyo itatoweka ndio mwisho wa utalii katika hifadhi hii ambayo inaiingizia serikali fedha nyingi za kigeni,” anasema Bw. Lufungulo.

Wakizungumzia hali ya uharibifu wa mazingira baadhi ya wananchi mkoani Kilimanjaro wanasema katika kipindi cha  miaka 50 iliyopita hakujawahi kutokea mabadiliko makubwa ya hali ya hewa, kama yaliyotokea mwaka huu 2012.

Wanasema katika kipindi cha miaka ya nyuma mkoa wa Kilimanjaro ulisifika kwa baridi kali, lakini kwa sasa unatisha kwa kuonekana kuwa na joto kali hali ambayo si ya kawaida.

Wanasema  kunahitajika nguvu za ziada katika kurudisha uoto wa asili katika mkoa wa Kilimanjaro, ikiwa ni pamoja na kuimarisha sheria za uhifadhi na utunzaji  wa mazingira na endapo hayo hayatazingatiwa barafu ya mlima Kilimanjaro ambayo ndiyo mhimili wa mlima huo itapotea.

“Lakini hii inauma, kwani barafu inayoonekana katika kilele cha mlima Kilimanjaro inasemekana itakuja kuisha kama watanzania wote hatutachukua hatua za haraka za utunzaji wa mazingira na uoto wake wa asili, na hili ni dhahiri, kwani zamani maji yalikuwa yakitiririka kipindi chote cha mwaka, tofauti na sasa hivi ambapo yanatiririka kwa msimu  huku  joto  likiwa kali,” anasema Bw. Dastan Mongi.

Anawataka wananchi wanaoishi maeneo ya kuzunguka hifadhi ya Kilimanjaro kutowafumbia macho wananchi wanaoingiza mifugo katika hifadhi wala wanaoshiriki katika uvunaji miti.

“Nawaomba sana wananchi wa maeneo ya kuzunguka mlima Kilimanjaro wawe walinzi wa mlima huu na wasisite wala kuogopa kuwataja waziwazi watu wanaohusika kuuhujumu mlima huu kwa kukata miti na kulisha mifugo  hata kama ni kiongozi wewe ukimuona toa taarifa ili hatua kali zichukuliwe,” anasema Bw. Mongi.

“Ninyi wananchi wapasua mbao wako miongoni mwetu tunawajua, lakini hatuwasemi na wanaoingiza mifugo tunaishi nao, tushirikiane jamani na serikali ili kudhibiti tatizo la uharibifu wa mazingira ya mlima kwani kwa sasa tunaona mzaha lakini baadae tutaona  faida ya kudhibiti tatizo hili,” anasema.

Bw.Mongi anawataka pia viongozi kuwa mstari wa mbele kudhibiti uharibifu wa mazingira katika mlima Kilimanjaro kutokana na kwamba hali hiyo ikiachwa iendelee iutachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu shughuli za kitalii.

Tafiti zinaonyesha kuwa barafu ya mlima Kilimanjaro imepungua kwa asilimia 85 toka mwaka 1912 hadi kufikia mwaka 2008 hali ambayo inaelezewa kuwa ni kutokana na uharibifu wa mazingira.



No comments:

Post a Comment